Steinmeier azitaka Iran, Saudi kuzungumza
19 Januari 2016Waziri Steinmeir alisema Ujerumani inataka kufanya kazi na Iran kusaidia kutuliza migogoro ya kikanda, kwa vile sasa taifa hilo limetoka katika kutengwa kimataifa, na pia kuzuwia uhasama kuongezeka kati yake na hasimu wake wa kikanda Saudi Arabia.
Iran ilitoka katika miaka kadhaa ya kutengwa mwishoni mwa wiki, baada ya Marekani, Umoja wa Ulaya na umoja wa Mataifa kuiondolea vikwazo kuhusiana na mpango wake wa nyuklia, chini ya makubaliano ya kimataifa yaliyoihusisha pia Ujerumani.
Steinmeier alisema Iran ni muhimu katika kuituliza kanda ya Mashariki ya Kati, akimaanisha migogoro nchini Syria na Yemen, na husuani vita vya Syria ambavyo vimekuwa suala kuu katika mgogoro wa wakimbizi wa Umoja wa Ulaya, uliosababisha mgawanyiko mkubwa ndani ya umoja huo juu ya namna ya kugawana mzigo wa wakimbizi wanaotokana na mgogoro huo.
Inawezekana kujenga imani
Mataifa ya ghuba ya Arabuni yakiwemo Saudi Arabia yanaituhumu Iran kwa kuwaunga mkono waasi wa Yemen na wanamgambo wanaoiunga mkono serikali ya Syria.
Uhasama uliongezeka mwezi huu pale Saudi Arabia ilipomnyonga mhubiri maarufu wa Kishia, na kusababisha hasira kutoka kwa Iran.
Steinmeier amesema uhasama huu hautatoweka ndani haraka, lakini inawezekana kujenga uaminifu baina ya mahasimu hao wa kanda.
"Nimefanya kazi katika nyanja ya sera ya kigeni na ndani kwa muda mrefu na nafahamu kuwa uhasama katika uhusiano kati ya Saudi Arabia na Iran hautaboreka ndani ya usiku mmoja.
Lakini pengine hatupaswi kuwashinikiza sana, lakini kama hatua ya kwanza pande mbili zinapaswa kutuliza hali ya sasa, na kutoiacha kuongezeka zaidi, na hapo ndiyo waanze kuzungumza baina yao," alisema Steinmeier wakati akizungumza na waandishi wa habari mjini Berlin.
Suluhu ya mgogoro wa wakimbizi
Waziri Steinmeier pia alizungumzia miito inayozidi kutolewa kutaka kufungwa kwa mipaka ya Ujerumani ili kupunguza mmiminiko wa wakimbizi, na kusema haitaleta suluhu ya mgogoro huo. Alikuwa akijibu hoja iliyotolewa na waziri wa usafiri wa serikali kuu ya Ujerumani Alexander Dobrindt, aliesema suala la kufunga mipaka halikwepeki.
Steinmeier alisema suluhu ya muda mrefu ya mgogoro huo inaweza kuletwa tu kupitia mpango w akuwahifadhi wakimbizi katika mataifa yote ya Umoja wa Ulaya, juhudi za pamoja kuimarisha ulinzi wa mipaka ya nje ya umoja huo na kutimiza ahadi ya msaada wa euro bilioni 3 kwa Uturuki, kuiwezesha kuwahudumia wakimbizi wa Syria wapatao milioni 2.2 walioko huko.
Kusawazisha mambo na Poland
Waziri Steinmeier alisema ataitemebelea Poland wiki hii kujaribu kurekebisha uhusiano wake na Ujerumani, ambao uliyumba kufuatia mzozo baina ya mataifa hayo jirani. Alisema atakutana na wawakilishi wa serikali ya poland siku ya Alhamisi, katika moyo wa maridhiano, kwa kuzingatia uzito wa ukaliaji wa kimabavu wa utawala wa kinazi kwenye uhusiano wao.
Ujerumani na Umoja wa Ulaya zimekosoa vikali sheria mpya zilizopitishwa nchini Poland, kuhusu mahakama ya katiba na vyombo vya habari, ambazo zinadaiwa kwenda kinyume na misingi ya Umoja wa Ulaya.
Mwandishi: Iddi Ssessanga/afpe,rtre, dpae
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman