Steinmeier azuru Israel na Palestina
2 Novemba 2007Sababu hasa ya waziri Frank-Walter Steinmeier kufanya safari hiyo ya wiki moja hadi nchi mbalimbali za Mashariki ya Kati hasa ilikuwa kutayarisha mkutano wa kilele kati ya Israel na Palestina utakaofanyika Marekani hivi karibuni. Waziri Steinmeier alilengea kufahamu misimamo ya nchi jirani ili kutathmini uwezekano wa mkutano huu kufanikiwa.
Lakini alipokutana na waziri mkuu wa Israel na vilevile katika mazungumzo na waziri wa mambo ya kigeni wa Israel, Zipi Livni, hao wawili waligusia suala jingine. Israel inataka kuungwa mkono na Ujerumani katika juhudi zake za kuiwekea Iran vikwazo vikali zaidi. Viongozi wa Israel walitaja pia juu ya uhusiano wa kiuchumi kati ya Iran na Ujerumani.
Baada ya mazungumzo hayo, waziri Steinmeier alisema alimuomba Ehud Olmert kutoangalia upande mmoja tu: “Ikiwa kuna kitu kimoja ambacho sisi tunaweza kujivunia kufanya ni kwamba ni sisi ambao tangu mwanzoni tulipinga kabisa mradi wa kinyuklia wa Iran na mara nyingi tulitoa mapendekezo au kufanya juhudi ili Iran ibadili msimamo wake.”
Waziri Steinmeier aliongeza kusema kwamba Ujerumani haipingi kabisa vikwazo viongezwe iwapo Iran haitatimiza masharti yaliyowekewa juu ya mradi wake wa Kinyuklia. Hapo, msimamo wa Ujerumani ni sawa na wa nchi nyingiea za Ulaya na Marekani.
Katika kuzungumzia matayarisho ya mkutano wa Mashariki ya Kati chini ya uwenyekiti wa Marekani, waziri Steinmeier aliweka wazi msimamo wa nchi za Umoja wa Ulaya, ambao si kuingilia kati katika mzozo kati ya Waisraeli na Wapalestina bali kutoa mapendekezo na kusaidia kuimarisha usalama Mashariki ya Kati. Kwa azma hiyo, Umoja wa Ulaya umeandaa mpango maalum uliopendekezwa na Frank-Walter Steinmeier. Waziri huyu alisema: “Nia yangu ni kuzuia hali ya kuwa na mapendekezo au mipango tofauti baada ya mkutano wa Marekani bila ya mipango hiyo kuambatana.”
Mpango wa Umoja wa Ulaya hauhusu misaada mipya ya kifedha, bali miradi fulani kwa Wapalestina inayolenga hasa kuboresha elimu, kuimarisha uchumi, kuwafundisha maofisa wa usalama, kuunda mfumo wa sheria pamoja na kuanzisha taasisi za kiserikali zilizo wazikatika maeneo ya Wapalestina.
Matarajio mbele ya mkutano wa kilele huko Marekani yalizungumziwa pia kwenye mkutano kati ya waziri Steinmeier na rais Mahmud Abbas wa Palestina pamoja waziri wao wa mambo ya kigeni Al Maliki na mpatanishi mkuu Erekat. Waziri Steinmeier alisisitiza kwamba Israel na Wapalestina wanapaswa kutoiwachia nafasi hiyo ya kusaka amani. Hadi sasa lakini siyo tarehe wala mahali au washiriki wa mkutano huo wanaojulikana kwa sababu bado kuna tofauti nyingi kati ya Israeli na Wapalestina. Kwenye ziara yake, waziri Steinmeier aliarifu pia kwamba serikali ya Ujerumani inatoa msaada wa dadhura wa Euro Millioni moja kwa familia maskini zinazoishi katika eneo la ukanda wa Gaza.