1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ujerumani yatakiwa kupinga itikadi kali za mrengo wa kulia

10 Novemba 2025

Rais wa Ujerumani Frank Walter Steinmeier amevitolea wito vyama vinavyofuata siasa za mrengo wa kushoto kuwajibika zaidi katika kupambana na itikadi kali za mrengo wa kulia.

Berlin, Ujerumani 09.11.2025
Rais wa Ujerumani Frank-Walter SteinmeierPicha: Maryam Majd/POOL/AFP/Getty Images

Ameyasema hayo wakati Ujerumani ikiadhimisha miaka 36 tangu kuanguka kwa ukuta wa Berlin, tukio lililolofungua njia ya kuungana tena kwa iliyokuwa Ujerumani Magharibi na Ujerumani Mashariki.

Katika hotuba aliyoitoa mjini Berlin Jumapili, Steinmeier ameonya kuwa ongezeko la itikadi kali za mrengo wa kulia linahatarisha demokrasia nchini humo. Amezungumzia kuhusu ongezeko la itikadi hizo katika mfumo wa chama kinachopinga wahamiaji  cha Alternative for Germany (AfD), ambacho kilipata asilimia 20.5 ya kura katika uchaguzi mkuu wa Februari na kushika nafasi ya pili.

Rais Steinmeier ametahadharisha pia kuwa itikadi kali za mrengo wa kulia zinauweka rehani ukuta ambao vyama vya kidemokrasia vimejijengea ili kujitenga na chama cha AfD . Amesema mada nyeti kama vile uhamiaji na usalama zinapaswa kuwa wazi kujadiliwa bila kuibua tuhuma za ubaguzi wa rangi.

Steinmeier ameyatoa matamshi hayo katika siku hiyo maalumu kwa Ujerumani inayotumiwa pia kukumbuka kuanzishwa kwa Jamhuri ya Ujerumani na kuadhimisha kumbukumbu ya ghasia za mwaka 1938 dhidi ya Wayahudi ambapo zaidi ya masinagogi 1200 yaliharibiwa Ujerumani.

Ongezeko la chuki dhidi ya Wayahudi latajwa

Aidha, amelaani ongezeko la chuki dhidi ya Wayahudi tangu mashambulizi yaliyofanywa na wanamgambo wa Hamas Oktoba 7, 2023 nchini Israel. Zaidi Steinmeier ametoa wito wa udhibiti zaidi wa mitandao ya kijamii na kutahadharisha kuwa mustakabali wa demokrasia nchini humo utaamuliwa mtandaoni. Hata hivyo amesema, kuhakikisha taratibu za kidemokrasia zinazingatiwa mitandaoni ni suala muhimu katika kuihifadhi demokrasia yenyewe. 

Ukuta wa BerlinPicha: Staff Sergeant F. Lee Cockran/Looks Film

Zaidi amebainisha kuwa demokrasia na uhuru nchini Ujerumani havijawahi kushambuliwa kama nyakati hizi tangu Iliyokuwa Ujerumani Mashariki na Ujerumani Magharibi zilipoungana. Steinmeier amezungumzia vitisho kutoka nje kutokana na vita vya Urusi dhidi ya Ukraine pamoja na vitisho vingine vya ndani vinavyotokana na itikadi kali za mrengo wa kulia.

Kadhalika amesisitiza kuwa Wajerumani walio wengi wanataka kuishi katika demokrasia na uhuru. Ametoa wito kwa Wajerumani kuendeleza demokrasia na mafanikio katika jamii huru na yenye uwazi.

Amehitimisha kwa kusisitiza kuwa, licha ya tofauti kati ya wazawa, wenye historia ya uhamiaji Wajerumani wote ni wamoja.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW