1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Steinmeier ziarani Tanzania

31 Oktoba 2023

Rais Frank-Walter Steinmeier wa Jamhuri ya Shirikisho la Ujerumani yuko ziarani katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambako amefanya mazungumzo na rais wa huko, Samia Suluhu Hassan, juu ya ushirikiano wa nchi zao.

Rais Samia Suluhu Hassan wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (kulia) akiwa na mgeni wake, Rais Frank-Walter Steinmeier wa Jamhuri ya Shirikisho la Ujerumani.
Rais Samia Suluhu Hassan wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (kulia) akiwa na mgeni wake, Rais Frank-Walter Steinmeier wa Jamhuri ya Shirikisho la Ujerumani.Picha: Katharina Kroll/DW

Marais hao walifanya mazungumzo siku ya Jumanne (Oktoba 31) katika Ikulu ya Magogoni jijini Dar es Salaam juu ya kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi na kijamii baina ya mataifa hayo mawili.

Akimkaribisha mgeni wake kwenye mkutano na waandishi wa habari, Rais Samia alisema kwamba uhusiano baina ya Tanzania na Ujerumani unafikia sasa miaka 60, ambapo ndani ya kipindi chote hicho "Ujerumani imekuwa rafiki mwema kwa watu wa Tanzania."

Soma zaidi: Steinmeier aondoka Ujerumani kuelekea Tanzania

Rais huyo wa Tanzania aliishukuru Ujerumani kwa kuchangia kwenye miradi kadhaa ya maendeleo nchini mwake, hasa kwenye eneo la afya, ukiwemo ujenzi wa hospitali za kisasa.

Katika mkutano huo, Rais Steimeier alisema amefurahishwa na kasi ya Rais Samia ya kujenga nchi katika mfumo wa utawala bora na wa kisheria na hivyo kuahidi "kuendelea kuwa washirika wa karibu wa Tanzania."

Ziara maeneo ya kihistoria

Siku ya Jumatano (Novemba 1) ziara, Rais Steinmeier na ujumbe wake walitegemewa kuelekea mkoani Songea kutembelea makumbusho ya Vita vya Majimaji vilivyopiganwa na wenyeji dhidi ya utawala katili wa Kijerumani wakati wa ukoloni.

Simulizi za vita ya Majimaji mjini Kilwa

03:30

This browser does not support the video element.

Awali, Rais Steimeier alisema nchi yake ilikuwa tayari kufanya mazungumzo na familia za jamaa waliopoteza maisha wakati vita hivyo na kuangalia namna ya kurudisha mabaki ya miili yao ambayo kwa sasa yamehifadhiwa kwenye makumbusho nchini Ujerumani.

Kuhusiana na hilo, Rais Samia alisema licha ya nchi yake inatambuwa kuwa "ya kale yamepita" lakini inafahamu haja ya kufungua majadiliano na kuona jinsia ya kuzungumza na familia zilizoathirika wakati wa vita vya Majimaji.

Kwa pamoja, marais hao wawili walizungumza pia namna ya kuendelea kukuza misingi ya haki za binaadamu, kujenga uwezo wa vijana kiuchumi kupitia dijitali, na kuimarisha demokrasia.

Imetayarishwa na Florence Majani/DW Dar es Salaam 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW