Steinmeir aelezea matumaini yake kwa Lebanon baada ya kukutana na rais mpya wa nchi hiyo.
1 Juni 2008Steinmeir amesema makubaliano ya Doha kati ya makundi ya Lebanon yaliomaliza mzozo wa miezi 18 wenye madhara kwa nchi hiyo ni hatua muhimu sana kukomesha mzozo huo.
Amesema kuchaguliwa kwa rais na kuundwa kwa serikali ni ishara za matumaini akisisitiza kwamba makubaliano hayo yanasema kwamba nguvu na silaha hazipaswi kutumiwa kututawa mzozo huo.
Steinmeir ameongeza kusema kwamba ni jambo la kutia moyo kwamba katika hotuba ya kuapishwa kwake Suleiman ameelezea kuunga mkono mahkama ya kimataifa kuwashtaki waliohusika na mauaji ya waziri mkuu wa zamani wa Lebanon Rafik Hariri na viongozi wengine wanaoipinga Syria.
Pia amesisitiza kwa nchi jirani ya Syria kutambuwa uhuru wa Lebanon kuanzia hivi sasa.
Beirut ni kituo cha kwanza cha ziara ya Mashariki ya Kati ya waziri huyo wa mambo ya nje wa Ujerumani ambayo pia itamfikisha Jerusalem nchini Israel na Ramalla Ukingo wa Magharibi.