1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaUkraine

Stoltenberg: Hakuna mwaliko rasmi wa Ukraine katika NATO

11 Julai 2023

Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky amekosoa kile alichokiita "upuuzi" wa kukosekana ratiba ya kuonesha muda wa nchi yake kupewa uwanachama wa Jumuiya ya Kujihami ya NATO. Mkuu wa NATO amesema hakuna ratiba kamili

Litauen | Nato-Gipfel in Vilnius | Nato-Generalsekretär Jens Stoltenberg
Picha: Ludovic Marin/AFP/Getty Images

Kauli hiyo imeongeza sauti za ukosoaji mkali katika mkutano wa kilele wa viongozi wa muungano huo wa kijeshi ambao unakusudia kuonyesha mshikamano katika kukabiliana na uvamizi wa Urusi nchini Ukraine.

Soma pia: NATO: Kuungwa mkono Ukraine ni jukumu muhimu

Matamshi  ya Zelensky huenda yakaibua upya mivutano katika mkutano wa kilele wa NATO, ikiwa ni muda mfupi tu baada ya kitendo cha nia njema kutoka kwa Uturuki iliyokubali kuendelea na utaratibu wa kuikaribisha Swedenkatika muungano huo wa kijeshi.

Maafisa wametayarisha pendekezo, ambalo halijatolewa rasmi, kuhusu uwezekano wa uwanachama wa Ukraine. Rais wa Marekani Joe Biden alielezea uungaji mkono wake wakati wa mkutano na Katibu Mkuu wa NATO Jens Stoltenberg, lakini Zelensky ameandika kwenye Twitter kuwa hajaridhishwa na hilo. Amesema wanawathamini washirika wao, lakini Ukraine inastahili heshima. Zelensky tayari amewasili Vilnius na anatarajiwa kukutana na Biden na viongozi wengine wa NATO hapo kesho.

Zelensky asema Ukraine inahitaji heshima ya washirika Picha: Georgi Paleykov/NurPhoto/picture alliance

Waziri wa ulinzi wa Ukraine Oleksii Reznikov amesema baada ya kuwasili Vilnius kuwa wanasubiri habari njema. "Unajua, lengo kuu ni kupata uwanachama kamili. Ndio maana sitawaambieni kwa sasa kwa sababu tutasubiri hadi kesho ili kujua itakavyokuwa."

Kumekuwepo na migawanyiko mikali ndani ya muungano huo kuhusu azma ya Ukraine kujiunga na NATO, ambayo iliahidiwa mwaka wa 2008.

Baadhi wanahofia kuwa kuileta Ukraine katika NATO kunaweza kutumika kama uchochezi zaidi kwa Urusi na wala sio kizuizi dhidi ya uchokozi wake. Jake Sullivan, mshauri wa Biden wa usalama wa taifa, amesema washirika wanajadili kwa usahihi mkondo wa Ukraine kujiunga na NATO.

Mgogoro kuhusu Ukraine unasimama tofauti na makubaliano yaliyopiganiwa kwa bidii kuukubalia uwanachama wa Sweden.

Urusi imesema kuwa itafanya maamuzi yake kulingana na jinsi NATO itakavyoingia haraka na kwa undani kwenye mipaka ya Sweden. Sergei Lavrov ni Waziri wa mambo ya nje wa Urusi "maslahi yote halali ya usalama ya Shirikisho la Urusi yatahakikishwa pamoja na hatua mwafaka. Tunajua ni hatua gani na jinsi ya kuzitekeleza."

Suala la Ukraine linatarajiwa kuugubika mkutano wa kilele wa viongozi wa NATOPicha: Andrew Caballero-Reynolds/Pool Photo via AP/picture alliance

Biden na Erdogan wanatarajiwa kukutana jioni hii, na haijafahamika jinsi baadhi ya masharti mengine ya Rais huyo wa Uturuki yatakavyotatuliwa. Amekuwa akitafuta ndege za kisasa za kivita za Kimarekani na njia ya kupata uwanachama wa Umoja wa Ulaya.

Baada ya kukamilika mkutano wa kilele wa NATO kesho Jumatano, Biden ataelekea Helsinki. Siku ya Alhamisi, atasherehekea kujiunga kwa Finland katika NATO, na kukutana na viongozi wa mataifa ya UIaya kaskazini. 

Na wakati hayo yakiendelea mjini Vilnius, Urusi imefanya leo mashambulizi katika mji mkuu wa Ukraine, Kyiv, bandari ya Bahari Nyeusi ya Odesa na eneo la kusini la Kherson. Hakuna vifo vilivyoripotiwa katika mashambulizi ya droni jana usiku mjini Kyiv na Odesa, lakini gavana wa Kherson Oleksandr Prokudin amesema mwanamke aliuawa katika Kijiji cha kusini cha Sofiivka na watu wawili wakajeruhiwa mjini Kherson.

afp, reuters, dpa

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW