Strauss-Kahn aachiwa kwa dhamana
20 Mei 2011Dominique Strauss-Kahn, ameachiliwa kwa dhamana baada ya kusota rumande kwa siku tano.
Hata hivyo ametakiwa kubakia mjini New York, baada ya kutoa fedha taslim, dola milioni moja na kuwekewa bima ya dhamana ya dola milioni tano.
Dhamana hiyo imekuja baada ya jopo la majaji kumfungulia mashtaka saba dhidi yake juu ya tuhuma za jaribio la kumnyanyasa kimapenzi na kujaribu kumbaka mhudumu wa hoteli ya Manhattan jumamosi iliyopita.
Tuhuma ambazo Strauss-Kahn mwenyewe amesema atapambana nazo.
Wakati huohuo, uamuzi wa kujiuzulu kwa Mkurugenzi huyo mtendaji wa -IMF- umeibua mjadala kuhusu ni nani anayeweza kumrithi.
Kansela wa Ujerumani Angela Merkel anataka tena mtu kutoka
barani Ulaya kuongoza chombo hicho, wakati China, ikiunga mkono miito ya mataifa ya bara la Asia ya kumchagua kiongozi mpya kutoka taifa linaloinukia kiuchumi.