Strauss-Kahn ashinikizwa ajiuzulu kama mkuu wa IMF
18 Mei 2011Mkuu wa shirika la fedha la kimataifa, IMF, Dominique Strauss Kahn ambaye huenda akaendelea kuzuiliwa gerezani kisiwani Rikers mjini New York hadi kiasi cha kutakiwa kufika tena mahakamani siku ya Ijumaa, sasa yupo kwenye uangalizi mkali kuhakikisha kuwa hajitoi uhai , ikiwa ni hatua ya tahadhari inayochukuliwa dhidi yake akiwa gerezani.
IMF imesema haijawasiliana na mkuu huyo tangu kukamatwa kwake, lakini inaamini kuwa ni muhimu kufanya hivyo hivi karibuni. Hata hivyo shinikizo dhidi ya Strauss Kahn zinatizamwa tofauti na rais wa kundi la mawaziri wa fedha wa Umoja wa Ulaya Jean Claude Juncker.
'Ili mradi Strauss Kahn hajajiuzulu na sipendekezi afanye hivyo, sio ustaarabu kwamba baadhi ya serikali zimeanzisha mjadala huo'.
Nchini Marekani, ambayo ni mshikadau mkuu wa IMF, wanasiasa wameanza kuuliza maswali kuhusu uwezekano wa kuhudumu kwake kama mkuu wa shirika hilo. Waziri wa fedha nchini Marekani,Timothy Geithner, amesema Strauss Kahn hayupo katika nafasi ya kuweza kuiongoza IMF, na ametoa wito wa kutajwa rasmi mkurugenzi mkuu wa muda. Geithner ndiye afisa wa kwanza nchini Marekani kutoa matamshi kuhusu mkuu huyo wa IMF, tangu alipokamatwa siku ya Jumamosi.
Nchi za Ulaya zina hamu ya kuendelea kuushikilia wadhifa huo mkuu kwenye IMF, lakini masoko yanayoinukia yanashinikiza kuuwania wadhifa huo. Brazil inaamini kuwa kiongozi mpya wa shirika hilo anapaswa kutoka nchi kubwa inayoinuka kisoko, lakini haina mpango wa kushinikiza wazi hoja hiyo kwa kuwa huenda Ulaya ikaendelea kuudhibiti wadhifa huo.
Kwa upande mwingine Strauss Kahn pia aliendelea kupoteza uungwaji mkono. Waziri wa fedha wa Australia, Maria Fekter akitoa mtazamo wake kuhusu hatma ya Strauss Kahn, alisema, 'Katika mtazamo wa hali ilivyo, kwamba alinyimwa dhamana, ni lazima atafakari kuwa huenda hali yake ikaleta madhara kwa shirika hilo'.
Nchini Ufaransa, rais Nicholas Sarkozy katika mkutano wa siri, aliwaomba wabunge wa mrengo wa kulia, kujizuia kutoa matamshi kuhusu kesi dhidi ya Strauss Kahn. Viongozi wengi wa kisoshalisti walioneshwa kughadhabishwa kwao kwa jinsi mkuu huyo wa IMF, ambaye pia anatazamwa kuwa mgombea wa mbele wa urais nchini humo, alivyooneshwa mbele ya vyombo vya habari kabla ya kupewa fursa ya kujitetea mahakamani.
Meya wa jimbo la New York, Micheal Bloomberg, aliitetea hatua hiyo akisema, 'Ni aibu, lakini iwapo mtu hataki kuwasilishwa kihalifu, basi na asitende uhalifu'.
Mpaka sasa Strauss Kahn hajajiuzulu wadhifa wake huo kama mkuu wa shirika hilo la fedha la kimataifa, na pia hajajitoa kwenye kinyang'anyiro cha kugombea urais nchini Ufaransa. Viongozi wa kisoshalisti nchini humo, wamekubaliana kuwa hawatofanya mageuzi ya mpangilio wa uteuzi unaowataka wagombea kujisajili ifikapo Julai 13, kwa uchaguzi wa awali unaotarajiwa kufanyika mwezi Oktoba.
Mwandishi: Maryam Abdalla/Rtre/Dpae/Ape
Mhariri:Josephat Charo