Strauss Kahn na wadhifa wa mkurugenzi mkuu wa IMF
21 Septemba 2007Waziri wa zamani wa uchumi kutoka chama cha kisoshialisti cha Ufaransa,Dominique Strauss-Kahn ameiweka kando tama ya kua rais nchini mwake na kuahidi kuwajibika kwa muda wote wa miaka mitano atakayoongoza shirika la fedha la kimataifa IMF.
Mageuzi yanayohitajika katika kutekeleza shughuli za shirika la fedha la kimataifa IMF”hayatawezekana kufumba na kufumbua”.Patahitajika angalao mhula mmoja wa miaka mitano ambao nnahidi kuwajibika ipasavyo” amesema hayo Dominique Strauss-Kahn alipokua akihojiwa na wasimamizi wa shirika hilo katika makao yake makuu mjini Washington.
Domonique Strauss Kahn,aliyewahi kua waziri wa uchumi na fedha wa Ufaransa alikua mmojawapo wa watetezi watatu wakuu wa kutoka chama cha kisoshialisti waliokua wakifikiria kupigania wadhifa wa rais nchini mwake,uchaguzi ulipoitishwa mwezi May uliopita.Wanaharakati wa chama cha kisoshialisti lakini wakaamua kumtanguliza mbele bibi Ségolène Royal .
Bibi Royal alishindwa na rais Nicolas Sarkozy.
Uchaguzi mpya wa rais nchini Ufaransa utafanyika msimu wa kiangazi mwaka 2012.Ikiwa Strauss-Kahn atataka kutetea tena wadhifa huo,basi atalazimika kuacha wadhifa wake kama mkurugenzi mkuu wa shirika la fedha la kimataifa angalao mwaka mmoja kabla ili kuweza kuteuliwa na chama chake na kuendesha kampeni yake ya uchaguzi.
Akiulizwa suala hilo baada ya kuhojiwa na wasimamizi wa shirika la fedha la kimataifa,Dominique Strauss Kahn hakusema kinaga ubaga kama hatopigania wadhifa huo.Jibu lake lilikua tunanukuu:”Miaka mitano ndio muda wa wadhifa huu na ukichaguliwa kwa muda wa miaka mitano,huwezi kusema unaondoka baada ya miezi sita”-mwisho wa kumnukuu.
Alikua rais wa Ufaransa Nicolas Sarkozy aliyemteuwa Dominique Strauss Kahn kupigania wadhifa wa mkurugenzi mkuu wa shirika la fedha la kimataifa IMF,akimsifu kua mtu “mwenye sifa za kila aina, ujuzi na maarifa”.
“Dominique Strauss Kahn ana fikra sawa na zangu kuhusiana na IMF na nitamfanyia kampeni ili achaguliwe kua mkurugenzi mkuu wa IMF,alishadidia rais huyo wa Ufaransa,mwezi July uliopita.
Alipohojiwa na wasimamizi wa IMF mjini Washington,Dominique Strauss Kahn,mwenye umri wa miaka 58 amesema” kuwepo shirika la IMF kunabishwa vikali na mashirika yanayopinga mfumo wa soko huru na yale yanayopinga utandawazi”.Jukumu la mkurugenzi mkuu mpya litakua kurejesha hali itakayoliwezesha shirika la IMF kuaminika.”
Baada ya kuonana na viongozi kadhaa na hasa wa nchi zinazoinukia,katika kile alichokiita “ziara ya kilomita laki moja”,waziri huyo wa zamani wa uchumi na fedha wa Ufaransa amesema ameshangazwa kuona jinsi shirika hilo lilivyofika njia panda.
Kishindo kikubwa kilichopo ni kama shirika hili litaendelea kuangaliwa kama taasisi muhimu yenye kusimamia utulivu wa fedha ulimwenguni amesema bwana Strauss Kahn.
Amesema jukumu la IMF halikubadilika tangu shirika hilo lilipoasisiwa baada ya vita vikuu vya pili vya dunia,katika wakati ambapo hali ya mambo hivi sasa imebadilika moja kwa moja katika enzi hizi za utandawazi.IMF lazma ishikilie nafasi muhimu katika hali ambayo ni kinyume na ile iliyokuwepo hapo zamani.”Amesema Dominique Strauss Kahn aliyesisitiza tunanukuu” hataki kua mtetezi wa nchi za kaskazini dhidi ya nchi za kusini au wa nchi tajiri dhidi ya maskini.
Domonique Strauss Kahn anaungwa mkono na nchi zote 27 za Umoja wa ulaya na Marekani pia.
Anapewa nafasi nzuri ya kumshinda mtetezi wa Urusi Tosovsky,wanachama wa baraza la shirika la fedha la kimataifa watakapokutana kumteuwa mkurugenzi mkuu mpya September 28 ijayo.