1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Stuttgart yalenga kumaliza kazi dhidi ya Hamburg

5 Juni 2023

Stuttgart wana faida nono ya mabao matatu kwa sifuri kutokana na mkondo wa kwanza wa mechi yao ya mchujo ya kuamua atakayepandishwa au kushushwa daraja katika Bundesliga dhidi ya Hamburger SV

Fussball, Relegation, Bundesliga, VfB Stuttgart - Hamburger SV
Picha: Heiko Becker/HMB Media/picture alliance

Lakini mkondo wa pili unachezwa leo usiku katika dimba la Hamburg mbele ya mashabiki 57,000. Kama Stuttgart watafaulu kuhimili kishindo cha Hamburg, basi watabaki katika Bundesliga kwa msimu wa nne mfululizo. Stuttgart walimaliza katika nafasi ya 16 kwenye msimamo wa Bundesliga, na kwa hiyo watahitaji kuwashinda Hamburg, waliomaliza katika nafasi ya tatu katika ligi daraja la pili. Vilabu vya Heidenheim na Darmstadt vilipata tiketi za kupanda moja kwa moja katika Bundesliga wakati Schalke na Hertha Berlin zikiteremka.

Leipzig wabeba Kombe la DFB Pokal

Karibu mashabiki 8,000 waliikaribisha nyumbani jana RB Leipzig na kushereherekea na timu yao taji la Kombe la Shirikisho la Ujerumani – DFB Pokal. Leipzig walishinda taji hilo kwa mara ya pili mfululizo baada ya ushindi wa 2 – 0 dhidi ya Eintracht Frankfurt katika dimba la Olimpiki mjini Berlin. Kikosi hicho kililipeleka kombe hilo katika ofisi za Baraza la Jiji kabla ya msafara kuelekea katika dimba lao la Red Bull Arena.

Kombe hilo la kwanza katika kandanda la Ujerumani ndio mafanikio makubwa ya kocha Marco Rose, na thibitisho kuwa yeye ndiye mtu sahihi wa kuifundisha klabu hiyo. Ameiongoza timu hiyo kumaliza katika nafasi ya tatu na kufuzu katika Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao. Hata hivyo, watastahili kujipanga upya maana wachezaji wao nyota Christopher Nkunku na Konrad Laimer wanahama. Nkunku anaelekea Chelsea ya Premier League wakati Laimer anatimkia kwa mahasimu wao Bayern Munich.

afp/reuters/dpa/ap