1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Sudan: Waandamanaji wahofia mpango wa kuwasambaratisha

Zainab Aziz Mhariri: Yusuf Saumu
15 Aprili 2019

Wapinzani nchini Sudan wamesema pana mpango wa kuzivuruga harakati zao. Chama cha watalaamu kinachoongoza maandamano kimetoa wito kwa wananchi kujiunga na kampeni hiyo mbele ili kuyalinda mapinduzi ya wananchi.

Sudan Protest vor Militärhauptquartier in Khartum
Picha: Getty Images/AFP/A. Shazly

Chama hicho kimetoa wito huo kwenye mtandao wake wa kijamii wakati ambapo watawala wa kijeshi wa Sudan wanakabiliwa na shinikizo kubwa la waandamanaji na miito inayotolewa na serikali za nchi za magharibi kuwataka watawala wao wakabidhi mamlaka kwa raia.

Kwa mujibu wa mwandishi wa shirika la habari la AFP aliyehudhuria mkutano kati ya baraza la kijeshi na wawakilishi wa vyama vya kisiasa, amesema baraza hilo la kijeshi limewahimiza wanasiasa wakubaliane juu ya mtu anayeweza kuwa waziri mkuu.

Waandaaji wa maandamano hayo walifanya mazungumzo kwa siku ya pili hapo jana Jumapili pamoja na wajumbe wa baraza la mpito la kijeshi, baada ya kulitaka jeshi likabidhi mamlaka ya kuongoza serikali ya mpito kwa muda wa miaka minne.

Leo inatimia siku ya kumi tangu maandamao makubwa yaanze kufanyika mbele ya makao makuu ya jeshi baada ya viongozi wa upinzani kutoa matamko ya kulitaka baraza la kijeshi likabidhi mamlaka kwa raia baada ya baraza hilo kumng'oa madarakani rais Omar al-Bashir.

Waandamanaji katika jiji la KhartoumPicha: Reuters

Viongozi wa upinzani ambao wamekuwa wanaongoza harakati za upinzani kwa muda wa miezi kadhaa sasa limesema serikali ya mpito pamoja na wanajeshi wanapaswa kuwachukulia hatua za kisheria Rais wa hapo awali Omar al-Bashir na maafisa wa idara zake za ujasusi zilizokuwa kitisho kwa wananchi. 

Marekani, Uingereza na Norway zimelitaka baraza la kijeshi la Sudan lianzishe mazungumzo na pande zote juu ya kutayarisha kipindi cha mpito kuelekea kwenye utawala wa kiraia. Katika tamko la pamoja la balozi za nchi hizo zimeonya dhidi ya matumizi ya nguvu kwa lengo la kuuzima upinzani wa wananchi. Nchi hizo  zimesema madai halali ya watu wa Sudan bado hayajatekelezwa.

Wakati huo huo baraza la kijeshi la Sudan leo Jumatatu limesema litafanya marekebisho katika halmashauri  kijeshi na limemteua Kanali jenerali Hashem Abdel Muttalib Ahmed Babakr kama mkuu wa majeshi. Kanali Mohamed Othman al-Hussein ameteuliwa kuwa naibu mkuu wa majeshi.

Vyanzo:/AFP/RTRE