1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Sudan: Burhan asema jeshi kutoa nafasi kwa serikali ya raia

5 Julai 2022

Kiongozi wa jeshi la Sudan Abdel Fattah al-Burhan amesema jeshi la nchi hiyo halitashiriki katika mazungumzo yanayoshinikzwa kimataifa ili kuondoa mkwamo wake na upinzani wa kiraia

Abdel-Fattah Burhan
Picha: Marwan Ali/AP/picture alliance

Katika hotuba hiyo iliyopeperushwa kupitia televisheni, Burhan ameyataka makundi ya kiraia kuanza mazungumzo ya kina ya kuirudisha nchi hiyo katika kipindi cha mpito cha kidemokrasia. Ameongeza kuwa jeshi litajitolea kutekeleza matokeo ya mazungumzo hayo. Burhan amesema kuwa baraza kuu la utawala analoliongoza linalojumuisha maafisa wa kijeshi na raia, litavunjiliwa mbali baada ya kuundwa kwa serikali mpya.

Burhan ameongeza kuwa baraza kuu jipya la kijeshi baadaye litaundwa na kuwajibikia majukumu ya kiusalama na ulinzi pamoja na majukumu mengine kwa makubaliano na serikali. Hata hivyo matamshi yake hayakufafanua jukumu la kisiasa liitakalochukuliwa na jeshi hilo kuendelea mbele. Tangazo hilo la la Burhan linakuja miezi kadhaa baada ya mapinduzi ya mwezi Oktoba yaliouondoa uongozi wa kiraia katika serikali ya mpito na kuzua shtuma za kimataifa na pia kukatizwa kwa msaada kwa taifa hilo ambalo limeshuhudia miingiliano ya nadra tu ya utawala wa kiraia.

Waandamanaji wasema hawakuvutiwa na hotuba ya Burhan

Hotuba hiyo pia imetolewa katika siku ya tano ya maandamano ya hivi karibuni zaidi ya kupinga mapinduzi hayo ya kijeshi baada ya maandamano ya Alhamisi kushuhudia ghasia mbaya zaidi mwaka huu. Shirika la reuters limeripoti kuwa takriban watu elfu 2 walishiriki katika maandamano hayo ya Jumatatu mchana . Hata hivyo waandamanaji hao hawakuvutiwa na maneno ya jenerali huyo, na katika wilaya ya Burri mjini Khartoum waandamanaji wapya walijitokeza mara moja.

Waandamanaji mjini Khartoum nchini SudanPicha: Marwan Ali/AP Photo/picture alliance

Mwandamanaji mmoja Muhannad Othman amesema kuwa hawana imani na Burhan na kwamba wanamtaka aondoke kabisa. Mwandamanaji mwengine Oumeima Hussein aliyekuwa katika eneo la katikati mwa Khartoum, amesema kuwa Burhan anapaswa kuhukumiwa kwa wale wote waliouawa tangu mapinduzi hayo na kuapa kwamba waandamanaji watamuondoa madarakani kama walivyomfanya Bashir.

Muungano wa FCC wajiandaa kwa jibu la hotuba ya Burhan

Shirika la habari la Ufaransa AFP limeripoti kuwa kufikia jana jioni, muungano wa kiraia wa Forces for Freedom and Change, FCC, uliandaa mkutano wa dharura kujadili kuhusu jibu kwa hotuba ya Burhan.

Kuondolewa madarakani kwa mbabe Omar al-Bashir mwaka 2019 baada ya maandamano makubwa, kulisababisha utawala wa mpito wa kiraia na jeshi. Wiki kadhaa baada ya mapinduzi hayo, viongozi ya kijeshi na kiraia waliahidi kufanya uchaguzi mkuu mnamo mwezi Julai mwaka 2023. Mwezi uliopita, wadau wakuu wa kiraia nchini humo, walikataa kushiriki katika mazungumzo na viongozi hao wa kijeshi yalioanzishwa kwa juhudi za kimataifa kudumisha kipindi hicho cha mpito.