Sudan, Ethiopia na Misri bado zavutana kuhusu mto Nile
22 Juni 2020Mivutano inazidi kuongezeka kati ya nchi hizo tatu baada ya mazungumzo ya hivi karibuni kushindwa kufikia makubaliano kuhusiana na mpango wa kulijaza maji na kuanza kazi kwa Bwawa la umeme nchini Ethiopia.
Waziri wa rasilimali za maji na umwagiliaji wa Sudan, Yasser Abbas amesema nchi yake haitaki malumbano bali inaamini kuwa mazungumzo ndiyo suluhisho la pekee. Abbas amesema kutiliana saini makubaliano ni sharti linalopasa kutiliwa maanani kabla ya kulijaza maji bwawa hilo na kwamba nchi yake Sudan ina haki ya kudai hilo. Ethiopia imetangaza mipango ya kuanza kulijaza bwawa hilo kubwa la kuzalisha umeme mwezi ujao, bila kujali iwapo makubalino juu ya mpango huo yamefikiwa au la.
Misiri, ambayo inauchukulia mradi wa umeme wa Ethiopia kama tishio kubwa kwa maslahi yake mnamo siku ya Ijumaa ilitoa mwito kwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuingilia kati mzozo huo huku ikiutaja msimamo wa Ethiopia kuwa usio sawa.
Misri inailaumu Ethiopia kwa kukosekana mafanikio ya kufikia makubaliano, ikisema kuwa nchi hiyo haina ari ya kutaka kufikia makubaliano ya kisiasa. Rais wa Misri, Abdel Fattah al-Sisi alisema katika hotuba yake kwa njia ya runinga kwamba nchi yake inataka na imeendelea kusimama imara kwa dhati juu ya kutafuta suluhisho la kisiasa kwa mzozo huo.
Kwa ombi la Misri, nchi za Jumuiya ya nchi za Kiarabu zitajadili suala hilo katika mkutano wa kawaida wa mawaziri wa mambo ya nje utakaofanyika siku ya Jumanne.
Misri inahofia kwamba bwawa hilo la umeme linaweza kupunguza mtiririko wa maji kutoka kwenye mto wa Nile kuelekea nchini Misri, maji ambayoyanakimu mahitaji ya maji safi ya Misri kwa karibu asilimia 97.
Ethiopia inasema bwawa hilo linahitajika kwa maendeleo yake na imesisitiza kwamba mtiririko wa maji kuelekea Misri hautaathiriwa. Mto wa Nile ni njia ya kusambaza maji na umeme kwa nchi 10 ambazo maji hayo yanapitia. Misiri inautegemea Mto Nile kwa shughuli za kilimo, viwanda na matumizi ya maji ya ndani hata hivyo Ethiopia imesema wasiwasi wa Misri hauna msingi.
Ethiopia ilianza kujenga bwawahilo la umeme litakalogharimu dola bilioni 4.8 mnamo mwaka 2010, kama sehemu ya mpango wake wa kukuza mauzo yake ya nje ya nishati ya umeme.
Vyanzo:/DPA/AFP