1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Sudan: Haki yahitajika kwa mauaji ya waandamanaji

18 Novemba 2019

Shirika la kutetea haki za binaadamu Human Rights Watch limesema katika ripoti yake kwamba waliohusika na mashambulio mabaya dhidi ya waandamanaji Juni, 2019 nchini Sudan, wanapaswa kuwajibishwa kikamilifu.

Sudan Proteste in Khartum
Picha: Reuters/M. N. Abdallah

Ripoti hiyo iliyo na kurasa 59, inayozungumzia kamata kamata iliyofanywa na vikosi vya usalama mjini Khartoum  inaelezea namna maafisa wa usalama walivyowavamia waandamanaji waliokuwa wamepiga kambi katika mahema yao mjini humo Juni 3, 2019 na katika maeneo mengine jirani ya Bahri na Omdurman.

Shirika hilo  kupitia Jehanne Henry mkurugenzi wake wa eneo la Afrika, limesema serikali mpya ya mpito nchini Sudan inabidi ioneshe kwamba imejizatiti kuwawajibisha wale walioohusika katika mashambulio mabaya dhidi ya waandamanaji baada ya miongo kadhaa ya ukandamizaji na mateso dhidi ya raia wa nchi hiyo.

Shirika hilo la kutetea haki za binaadamu la Human Rights Watch limewahoji zaidi ya watu 60 wakiwemo waathiriwa wa uhalifu tofauti, kwa mfano waathirika wa unyanyasaji wa kingono, na walioshuhudia dhuluma hizo na pia kuangalia na kufanyia utafiti picha, video na kufuatilia jumbe katika mitandao ya kijamii.

Alfajiri ya tarehe 3 mwezi Juni siku ya mwisho ya mwezi mtukufu wa Ramadhani idadi kubwa ya vikosi  vya usalama viliyoongozwa na kikosi kinachoogopwa cha kupambana na ghasia RSF waliwamiminia risasi waandamanaji wasiokuwa  na silaha na kuwaua wengi wao papo hapo. Vikosi hivyo viliwabaka, kuwachoma visu, kuwapiga waandamanaji, kuwadhalilisha wengi kwa kuwakata nywele zao, kuwalazimisha kutambaa katika maji machafu, kuwakojolea pamoja na kuwatukana na kuiba na kuchoma mahema na mali nyengine katika eneo hilo.

Kupanda kwa bei ya mkate kulizua maandamano

Raia wa Sudan wakiandamana mjini KhartoumPicha: Reuters/M. N. Abdallah

Maandamano ya kitaifa yaliosababisha unyama huo, yalianza nje kidogo ya mji wa Khartoum katikati ya mwezi Desemba mwaka 2018, kufuatia kupanda kwa bei ya mkate, na baadae kugeuka na kuwa maandamano dhidi ya utawala wa miaka 30 wa Omar al Bashir. Waandamanaji baadae walipiga kambi katika makao makuu ya jeshi mwezi Aprili na kusababisha Rais Omar al Bashir kuondolewa madarakani Aprili 11. Baraza la kijeshi lilichukua madaraka na waandamanaji wakaendelea na maandamano hayo wakitaka sasa jeshi likabidhi madaraka kwa raia.

Maandamano hayo nayo yakasababisha mauaji mengine mengi ya waandamanaji mwezi May na Aprili, yaliolaaniwa na Umoja wa Ulaya, Marekani, Uingereza na Norway. Na Umoja wa Afrika nao ukataka uchunguzi wa kina ufanyike dhidi ya mauaji hayo. Lakini matokeo yake serikali ya Sudan ikakanusha mashambulio hayo.

Baada ya shinikizo kutoka kila upande wa dunia kutaka suluhu la mgogoro wa kisiasa upatikane, viongozi wa kijeshi na wale wa upinzani wakakubaliana mnamo Agosti 17 kuwa na serikali ya mpito itakayoongozwa na pande zote mbili kijeshi na kiraia, itakayoongozwa na Waziri Mkuu mpya Abdalla Hamdok.

Kama ilivyokubalika Hamdok akateua kamati itakayochunguza mauaji ya Juni 3 lakini makundi ya waathiriwa wakazua masuali ya kwamba kamati hiyo sio huru isiowajumuisha wanawake au hata wataalamu wa unyanyasaji wa kingono. Na ndio maana shirika la HRW linataka serikali ya sasa kuiangalia upya kamati hiyo au kuteua kamati mbadala itakayokuwa na uhuru wa kuchunguza mauaji na kuwawajibisha wale wote watakaopatikana na hatia bila kujali vyeo vyao.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW