1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaSudan

Umoja wa Mataifa waonya juu ya hali tete, Darfur

11 Novemba 2023

Umoja wa Mataifa umeonya juu ya kuongezeka kwa ukiukwaji wa haki za binaadamu katika jimbo la Darfur nchini Sudan na kusema unaelekea kuwa "uovu".

Moshi ukifuka wakati mapigano kati ya jeshi la Sudan na wanamgambo wa RSF wanapoendelea kukabiliana nchini humo, hali inayozidi kuibua wasiwasi wa mzozo wa kibinaadamu
Moshi ukifuka wakati mapigano kati ya jeshi la Sudan na wanamgambo wa RSF wanapoendelea kukabiliana nchini humo, hali inayozidi kuibua wasiwasi wa mzozo wa kibinaadamuPicha: AFP

Umoja wa Mataifa unasema hayo wakati mapigano yaliyodumu kwa miezi saba yakizidi kushika kasi kati ya jeshi la Sudan na wanamgambo wa RSF.

Mratibu wa masuala ya kiutu wa Umoja huo nchini Sudan Clementine Nkweta-Salami amesema hali ni ya kutia wasiwasi na hawana namna zaidi ya kuielezea kuhusiana na kile kinachotokea nchini humo.

Amesema bado wanaarifiwa juu ya visa vya unyanyasaji wa kutisha wa ngono, watu kupotezwa kinguvu, vifungo vya kiholela na ukiukwaji mkubwa wa haki za binaadamu na watoto.

Mratibu huyo aidha ameonya juu ya mashaka ya mauaji ya kimbari kutokea tena kama ya miaka ya 2000 kwenye jimbo hilo la Darfur.