Sudan: Jeshi lachukua udhibiti wa jengo la shirika la habari
13 Machi 2024Jengo la shirika la utangazaji la serikali liko Omdurman, mji unaopakana na mto Nile na ambao ni moja ya sehemu pana ya mji mkuu Khartoum. Mji huo umeshuhudia mapigano makali karibu na kambi za kijeshi, madaraja na njia za usambazaji.
Mapigano yameendelea licha ya miito ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ya kuzitaka pande hizo zinazohasimiana kuweka chini silaha ili kuruhusu misaada ya kibinadamu nchini humo hasa wakati huu wa mwezi mtukufu wa Ramadhan ulioanza sik ya Jumatatu.
Soma pia: Guterres ataka usitishaji mapigano Gaza, Sudan
Wito wa kusitisha mapigano ulipokewa kwa mikono miwili na wanamgambo wa RSF, japo ulikataliwa na jenerali mmoja mkuu katika jeshi la Sudan. Hivi karibuni, jeshi hilo limedai kupata mafanikio japo kidogo katika mji wa Omdurman baada ya kuonekana kulemewa na RSF kwa muda mrefu.
Hatua ya jeshi kuchukua udhibiti wa jengo la makao makuu ya shirika la utangazaji la serikali kutaongeza udhibiti wake kwenye maeneo yote ya kaskazini mwa Omdurman japo mahasimu wao RSF wanadhibiti sehemu za kusini na magharibi mwa mji huo.
Wafuasi wa jeshi la Sudan washerehekea
Vidio iliyochapishwa na jeshi jana Jumanne, katika eneo ambalo lilithibitishwa na shirika la habari la Reuters, ilionyesha baadhi ya wanajeshi wa Sudan wakishangilia wakiwa karibu na umbali wa angalau kilomita moja kutoka majengo ya kituo cha redio na televisheni ya taifa.
Katika mitandao ya kijamii, wafuasi wa jeshi pia walishangilia kwa kile walichokiita, ukombozi wa "sauti ya taifa."
Huyu ni mmoja wa watangazaji waliofurahia hatua hiyo ya jeshi.
"Kuurudisha moyo mahali pake sahihi ili uendelee kufanya kazi. Asante jeshi la Sudan kwa kuturudishia pumzi ambazo zilikuwa zimekatika tangu wanamgambo wa RSF walipokalia jengo hili lenye redio na televisheni.”
Mashuhuda wamesema jeshi la Sudan, ambalo limekuwa likitegemea uimara wao katika anga na zana nzito za kivita kukabiliana na RSF, sasa limepeleka ndege zisizo na rubani katika mji huo wa Omdurman kujaribu kupanua udhibiti wao.
Hata hivyo, hakukuwa na kauli yoyote kutoka RSF.
Soma pia: Jeshi la Sudan lakataa kusitisha mapigano mwezi wa Ramadhani
Wanamgambo hao wa RSF walichukua udhibiti wa jengo la makao makuu ya shirika la utangazaji la serikali wakati kulipozuka mapigano katikati ya mwezi Aprili mwaka jana, na walikitumia chombo hicho cha habari pamoja na taasisi nyengine za umma kwa ajili ya shughuli zao za kijeshi.
Mapigano kati ya jeshi la Sudan na kundi la RSF yalizuka katikati ya msuguano kuhusu mpango wa mpito kuelekea utawala wa kiraia.
Vita nchini Sudan vimeuharibu mji mkuu Khartoum na kusababisha mauaji yaliyochochewa kikabila katika eneo la magharibi la Darfur. Sio hayo tu, vita hivyo pia vimesababisha mzozo mkubwa zaidi wa kibinadamu.