1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Sudan: Jeshi na upinzani wakubaliana kuunda baraza la mpito

Daniel Gakuba
28 Aprili 2019

Watawala wa kijeshi nchini Sudan wamepata makubaliano na viongozi wa upinzani juu ya kuundwa kwa baraza la mpito linalojumuisha wanajeshi na raia. Mitaani, maandamano yameendelea kulishinikiza jeshi kukabidhi madaraka.

Sudan l nach Putsch l  Proteste gegen Militärrat
Picha: Getty Images/AFP/O. Kose

Baraza la kijeshi lililochukua madaraka baada ya kuuangusha utawala wa muda mrefu wa Rais Omar al-Bashir pamoja na muungano wa upinzani, walifanikiwa Jumamosi kupata muafaka juu ya kuundwa kwa baraza la uongozi wa mpito, lenye wajumbe kutoka jeshi na upinzani wa kiraia. Baraza hilo la kijeshi lenye wajumbe 10 lilikuwa limejitwisha majukumu ya kuongoza kipindi cha mpito cha miaka miwili, baada ya kumuondoa madarakani al-Bashir Aprili 11 kufuatia wimbi kubwa la maandamano ya umma kupinga utawala wake wa miongo mitatu.

Muungano wa upinzani ujulikanao kama 'Azimio la Uhuru na Mabadiliko' ambao unaongozwa na chama cha wanataaluma nchini Sudan ulianzisha mandamano makubwa  yaliyotaka utawala wa nchi uwekwe mikononi mwa raia, na kushinikiza kurejeshwa kwa demokrasia nchini mwao.

Soma zaidiRaia Sudan wasema mandamano yatadumu 

Baada ya kukubaliana kimsingi siku ya Jumatano kuunda kamati ya pamoja ya kushughulikia mizozo ya kisiasa, pande hizo mbili; jeshi na upinzani, Jumamosi zilifikia makubaliano ya kuunda baraza la pamoja la mpito. Mkutano wa Jumatano uliifuatiwa na kujiuzulu kwa maafisa watatu wa kijeshi kutoka baraza la mpito, ambao walishutumiwa kuwauwa waandamanaji na kuonekana kama wawakilishi wa serikali iliyoangushwa.

Baraza la pamoja la wanajeshi na raia

Kiongozi wa Baraza la Kijeshi Sudan, Abdel-Fattah al-BurhanPicha: picture-alliance/AA

Katika mkutano wa Jumamosi, hakuna makubaliano yaliyofikiwa kuhusu idadi ya viti vitakavyoshikiliwa na kila upande katika baraza hilo la pamoja la mpito. Mmoja wa viongozi wa waandamanaji, Ahmed al-Rabia ambaye alishiriki katika mazungumzo ya awali ya kuunda kamati mpya, aliliambia shirika la habari la AFP kuwa ''hivi sasa tunafanya majadiliano kuhusu asilimia ya viti vitakavyochukuliwa na wanajeshi, na vile vitakavyokaliwa na viongozi wa kiraia.''

Wakati hatua hiyo ikipigwa, maandamano makubwa yalikuwa yakiendelea mbele ya makao makuu ya jeshi mjini Khartoum, kulitia kishindo jeshi hilo liridhie kukabidhi uongozi kwa serikali ya kiraia. Wanaharakati wanahofu kwamba wanajeshi pamoja na washirika wa al-Bashir wataendelea kuidhibiti nchi, ikimaanisha kwamba mtawala mwanajeshi wa kiimla atakuwa amerithiwa na mwingine wa namna hiyo.

Soma zaidi: Omar al Bashir ahamishwa katika jela la Kobar

Baraza la mpito la kijeshi limewakamata baadhi ya maafisa waandamamizi wa serikali ya Omar al-Bashir , na kutangaza operesheni ya kupambana na ufisadi, na vile vile likitoa ahadi ya kurejesha madaraka kwa viongozi wa kiraia. Hata hivyo, limeshikilia azma ya kuwa na kauli ya mwisho katika maamuzi ya utawala wa nchi.

Sudan kwenye ukingo wa mabadiliko: lakini vipi upande wa uchumi?

Waandamanaji wameendelea kujimwaga mitaani, wakitaka jeshi likabidhi madaraka kwa raiaPicha: Getty Images/AFP/A. Mustafa

Serikali za nchi za Magharibi zinaunga mkono madai ya upinzani kutaka serikali ya kiraia, lakini Saudi Arabia na Umoja wa Falme za Kiarabu zimeendelea kutoa msaada wa kiuchumi kwa baraza la kijeshi la mpito linaloongozwa na Luteni Jenerali Abdel-Fattah al-Burhan. Uturuki na Qatar ambazo ni wapinzani wa mataifa ya Ghuba ya Uarabu, nazo pia zinanuia kulinda maslahi yake ndani ya Sudan mnamo wakati huu wa mabadiliko ya kisiasa.

Wakati huo huo, Rais wa Misri Abdel-Fattah al-Sisi ambaye ni mshirika wa karibu wa nchi za Ghuba ya Uarabu, na mwenyekiti wa sasa wa Umoja wa Afrika, amesema unahitajika muda kabla ya kuwekwa kwa serikali ya kiraia, ili kuepusha ghasia.

afpe, rtre