1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaSudan

Sudan: Wagner na vita vya kuwania madaraka na dhahabu

2 Mei 2023

Mamluki wa kundi la kijeshi la Urusi la Wagner wanaonekana kufanya kazi kwa karibu na utawala wa kijeshi nchini Sudan. Mabilioni ya dola yanadaiwa kutoroshwa ili kupata uungwaji mkono wa kisiasa na kijeshi wa Kremlin.

Afrika Wagner group in Mali
Picha: French Army/AP/picture alliance

"Warusi wananunua karibu kila kitu," Omar Sheriff, mchimba madini katika mji wa kaskazini-mashariki mwa Sudan wa Al-Ibaidiya, aliiambia DW muda mfupi kabla ya mzozo wa sasa kati ya wanajeshi wa Sudan na kundi la wanamgambo wa Rapid Support Forces (RSF) kuanza.

Sheriff ni mmoja wa wachimba migodi kadhaa huko Al-Ibaidiya, mji ulio kwenye ukingo wa Mto Nile ulioko takriban kilomita 400 kaskazini mwa mji mkuu Khartoum, ambao wanafanya kazi katika joto kali kukata dhahabu kutoka kwenye mawe jangwani. Hutenganisha dhahabu na miamba kwa kutumia michakato ya kemikali inayohusisha vitu vya sumu kama vile sianidi inayochuja na zebaki ambayo inaweza kuwadhuru wachimbaji na mazingira.

Soma pia: Mapigano makali kati ya majenerali hasimu yaendelea Sudan

Sehemu kubwa ya dhahabu hiyo huishia kwenye kiwanda cha kusindika kilicho umbali wa kilomita 16 kinachoendeshwa na kampuni inayomilikiwa na mwanzilishi wa kundi la mamluki wa Kirusi la Wanajeshi, Yevgeny Prigozhin, rafiki wa karibu wa Rais wa Urusi Vladimir Putin.

Kiongozi wa Kampuni ya kijeshi ya Wagner, Yevgeny Prigozhin.Picha: Konkord Company Press Service/ITAR-TASS/IMAGO

"Warusi wanaweza kulipa karibu dola 4,000 kwa lori la dhahabu," anasema Sheriff. "Mara nyingi wanatamani kununua kila kitu."

Wagner iliingia Sudan kwa mwaliko wa dikteta

Kundi la Wagner liliibuka kwa mara ya kwanza nchini Sudan mnamo 2017 kwa mwaliko wa Rais wa wakati huo Omar al-Bashir kufuatia mkutano kati ya dikteta wa Sudan na Putin huko Moscow.

Shirika hilo la jeshi kibinafsi lilianzisha kampuni ya Meroe Gold, inayodhibitiwa na Prigozhin ambayo baadaye iliwekewa vikwazo na Marekani, kuendesha shughuli zake katika taifa hilo la Afrika. Muda mfupi baadaye, ilianza kufanya utafiti wa rasilimali za dhahabu za Sudan.

Katika mchakato huo, Wagner alianza kujenga uhusiano na Jenerali Mohammed Hamdan Dagalo, anayejulikana kama Hemeti, na kikosi chake cha wanamgambo cha RSF.

Wanachama wa RSF, kulingana na wenyeji wa Al-Ibaidiya, walitoa ulinzi kwa wafanyabiashara wa Urusi ambao walitaka kununua dhahabu kutoka kwa wachimbaji madini.

Kiwanda cha kuchakata dhahabu kinachomilikiwa na Urusi pia kinasemekana kulindwa na wanamgambo kadhaa wa RSF ambao wanafanya kazi kwa karibu na mafisa usalama wa Urusi wanaoaminika kuwa kutoka Kundi la Wagner.

Soma pia: Umoja wa Mataifa watahadharisha kuhusu mgogoro wa wakimbizi Sudan

"Kwa zaidi ya miaka minne tumeona wanajeshi wa RSF wakifanya kazi kwa karibu na Warusi," Mustafa El Tahir, ambaye amekuwa akichimba dhahabu huko al-Ibaidiya tangu 2018, aliiambia DW. "Popote ambapo Warusi wanakwenda, RSF huenda nao."

Wagner ilidumisha uhusiano wake na Hemeti baada ya vuguvugu la kuunga mkono demokrasia la Sudan kumuondoa al-Bashir mwaka wa 2019.

Mnamo mwaka 2021, karibu tani 32.7 za dhahabu ya Sudan inayokadiriwa kuwa na thamani ya dola bilioni 1.9 iliripotiwa kutotolewa maelezo.Picha: Ashraf Shazly/AFP/Getty Images

Kuondolewa kwake kulifungua njia kwa serikali ya mpito ya kiraia. Uhusiano huo ulionekana kuwa muhimu katika kupindua serikali inayoongozwa na raia karibu miaka miwili baadaye.

Kufuatia mapinduzi hayo, yanayodaiwa kuungwa mkono na Urusi, Jenerali wa jeshi Abdel Fattah Burhan alichukua nafasi ya kiongozi wa kijeshi na kumfanya Hemeti kuwa naibu wake.

Ndege yenye dhahabu safi

Tangu jeshi kurejea madarakani, ushirikiano wa Wagner na Hemeti umeshika kasi. Mnamo Februari 2022, Urusi ilipoanzisha uvamizi wake nchini Ukraine, Hemeti alisafiri hadi Moscow ili kuunga mkono mipango ya Urusi ya kuanzisha kituo cha jeshi la wanamaji kwenye Bahari ya Sham, hatua ambayo Burhan alikataa kuidhinisha.

Katika safari hiyo ya Urusi, ndege aliyosafiria Hemeti pia ilikuwa ikisafirisha dhahabu iliyosafishwa, kulingana na New York Times, likiwanukuu maafisa wawili wakuu wa Magharibi. Wakati wa mazungumzo hayo mjini Moscow, Hemeti aliripotiwa kuomba msaada kutoka kwa maafisa wa Urusi ili kupata vifaa vya kijeshi.

Soma pia:WFP: Machafuko ya Sudan yanaweza kusababisha mgogoro wa kikanda

Mnamo mwaka wa 2021, kiasi cha tani 32.7 za dhahabu ya Sudan yenye thamani ya takriban dola bilioni 1.9 hazikujulikana zilipo, kulingana na ripoti ya shirika la utangazaji la Marekani CNN.

Ripoti hiyo pia imepata ushahidi unaoonyesha kuwa Urusi imefanya kazi kwa karibu na kikosi cha RSF cha Sudan ili kuhakikisha kuwa mabilioni ya dola ya dhahabu yanapita hazina ya Sudan ili kubadilishana na Kremlin uungwaji mkono wa kisiasa na kijeshi.

Mkuu wa jeshi la Sudan Abdel Fattah al-Burhan na mkuu wa RSF Mohammed Ahmad Daglo.Picha: Bandar Algaloud/Mahmoud Hjaj/AA/picture alliance

"Wakati wote, mpango huu mbovu unaohusisha Kundi la Wagner na serikali ya kijeshi umekuwa ukisimamiwa na Hemeti," anasema Ahmed Abdallah, mwanaharakati wa haki za binadamu wa Sudan aliye uhamishoni nchini Ujerumani.

"Siku zote unahisi kama wanaume wote [Hemeti na Burhan] hawakuwahi kuwa kwenye ukurasa mmoja kuhusu jinsi ya kufanya biashara na Wagner."

Sasa, ripoti mpya inaonyesha kwamba Wagner imekuwa ikiipatia RSF makombora kusaidia mapambano yao dhidi ya jeshi la Sudan.

Wiki iliyopita, CNN iliripoti kwamba kundi la uchunguzi la "All Eyes on Wagner" lilichambua picha za satelaiti ambazo zilionekana kuonyesha ndege ya usafirishaji ya Urusi ikiruka kati ya vituo viwili muhimu vya anga vya Libya vinavyodhibitiwa na Khalifa Hifter, kiongozi wa Jeshi la Kitaifa la Mashariki ya Libya, ambaye anaungwa mkono na Kundi la Wagner.

Shughuli za Wagner zasalia kuwa tata

Ripoti hiyo ilidai kuwa ongezeko la shughuli za Kundi la Wagner katika viwanja vya ndege vya kijeshi linaonyesha kuwa kulikuwa na mpango wa Urusi na Hafter kuunga mkono RSF hata kabla ya mzozo kuanza.

Soma pia: Matumaini mapya ya mazungumzo yachomoza Sudan licha ya mapigano kuendelea

"Nyuma ya harakati za Hemeti kunaweza kuwa Kundi la Wagner, ambalo wafanyakazi wake walikamatwa na kushutumiwa kwa ulanguzi wa dhahabu na serikali ya Burhan kabla tu ya mapigano kuanza," Yaser Abdulrehman, wakili wa Sudan aliiambia DW. "Hemeti na Wagner ni kama mapacha walioungana."

Lakini nia ya kweli ya Wagner Group inaonekana kubakia kutokuwa wazi.

"Wakati inaonekana kwamba Kundi la Wagner limetoa msaada wa kijeshi kwa Hemeti, ushiriki wa Wagner Group katika mzozo huu bado haueleweki," Isabella Currie, mtafiti wa Kundi la Wagner, aliiambia DW.

"Tahadhari inashauriwa katika kufikia hitimisho kuhusu uwezekano wa muungano kati ya Wagner na Hemeti, au jukumu la Wagner katika kuchochea machafuko ya wenyewe kwa wenyewe nchini Sudan. Kukosekana kwa utulivu nchini Sudan kunaweza kusiwe na manufaa kwa serikali ya Putin au mtandao wa Prigozhin, hasa kama mzozo utaanza kuathiri mpaka wa Sudan na Jamhuri ya Afrika ya Kati, ambapo Prigozhin imeanzisha uhusiano na kandarasi za uchimbaji rasilimali," alisema.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW