1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Sudan Kusini: Kiir na Machar wasaini makubaliano muhimu

Daniel Gakuba
4 Aprili 2022

Rais Salva Kiir na makamu wake Riek Machar wamefikia makubaliano ya kuunganisha uongozi wa jeshi la nchi hiyo, tukio linaloelezwa kama hatua muhimu kuelekea amani ya kudumu katika taifa hilo changa.

Wahlen Sudan Salva Kiir
(Picha ya maktaba) Rais Salva Kiir wa Sudan Kusini akisalimiana na afisa wa jeshiPicha: AP

Katika makubaliano hayo yaliyotiwa saini Jumapili mjini Juba, Rais Salva Kiir na makamu wake ambaye pia ni hasimu wake kisiasa, Riek Machar wameafikiana kuweka kamandi moja ya jeshi, suala ambalo linatajwa kuwa miongoni mwa vigingi vikubwa vilivyokuwa vinazuia kuheshimiwa kwa mapatano wa mwaka 2018 ya kuhitimisha miaka mitano ya vita vya wenyewe kwa wenyewe katika taifa hilo changa. 

Soma zaidi: Rais Kiir na Machar wakubaliana kuhusu usalama

Hivi karibuni, wanajeshi watiifu kwa Rais Kiir na vikosi vinavyoegemea upande wa Machar vimekuwa vikiendeleza chokochoko ambazo zilitiishia kuizamisha tena Sudan Kusini katika umwagaji mkubwa wa damu.

Kulipa gharama kwa ajili ya amani

Tut Gatluak, mshauri wa Rais Kiir katika masuala ya usalama alisema hatua iliyopigwa itawawezesha kutimiza matakwa ya raia wa Sudan Kusini.

(Picha ya Maktaba) Makamu wa Rais wa Sudan Kusini, Riek Machar (kushoto) akiwa na Katibu Mkuu wa zamani wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon Picha: picture alliance/dpa

''Leo hii tumekubaliana kuunganisha kamandi ya jeshi katika muundo wake ndani ya taasisi zote za usalama wa taifa, kwa ushirikiano na washirika wetu wa amani. Kwa vile amani ni ghali, tunapaswa kulipa gharama ili nchi ipate utengamano, na kufikia maendeleo yanayotarajiwa na wananchi,'' amesema Gatluak.

Soma zaidi:Amnesty: Vita vya Sudan vinaweza kuwa uhalifu wa kivita

Mbali na kuweka kamandi ya pamoja, pande hizo vile vile zimekubaliana kusitisha uhasama, na kukomesha propaganda zinazochochea mivutano. Hali kadhalika, mahasimu hao wameafikiana kusimamisha kampeni ya kuwashawishi wanachama wa upande mmoja kuhamia upande mwingine.

Bunduki zapaswa kunyamazishwa

Martin Gama Abucha aliyeyatia saini makubaliano ya jana kwa niaba ya Riek Machar, aliyasifu akiyaita hatua kubwa mbele, na kusisitiza lakini kuwa lililo muhimu zaidi kwa Wasudan Kusini ni kuona yaliyokubaliwa yakitekelezwa.

Ghasia za miaka mingi nchini Sudan Kusini zimewaletea taabu kubwa raia wa nchi hiyoPicha: Simon Wohlfahrt/AFP

Amesema, ''..kunyamaza kwa bunduki ndilo suala muhimu zidi kwa amani, hatuwezi kuendelea kuzungumzia amani huku tukiendelea kupigana. Bunduki zinapaswa kuwekwa chini, leo.''

Rais Salva Kiir na Riek Machar walihudhuria sherehe ya kuyasaini makubaliano hayo, ambayo yanaupa upande wa Kiir asilimia 60 ya nafasi za uongozi na 40 zilizosalia zikiiendea kambi ya Machar.

Soma zaidi:Mchakato wa amani unaoyumba Sudan Kusini wawasikitisha raia

Kwa mujibu wa makubaliano hayo, uteuzi wa kujaza nafasi zilizokubaliwa unapaswa kuwa umekamilika katika muda wa wiki moja, na jeshi litakuwa limeunganishwa katika kipindi kisichozidi miezi miwili.

Mchango mkubwa wa Sudan

Sudan ambayo ni mdhamini wa makubaliano ya amani ya mwaka 2018 nchini Sudan Kusini, iliwakilishwa na Mohamed Hamdan Daglo, namba mbili katika mpangilio wa madaraka kwenye baraza la kijeshi linaloitawala Sudan baada ya mapinduzi.

Umoja wa Mataifa ambao unao ujumbe wa amani nchini Sudan Kusini, umekuwa ukiwatuhumu wanasiasa wa nchi hiyo kuchochea kuchochea mivutano, kukanyaga uhuru wa watu na kutumia vibaya raslimali za nchi.

 

afpe, ape

 

Ruka sehemu inayofuata Gundua zaidi
Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW