1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroAfrika

Sudan Kusini: Itakuwaje UN isiporefusha marufuku ya silaha?

22 Mei 2025

Baraza la Usalama la UN litaamua mwishoni mwa Mei kuhusu kurefusha marufuku ya silaha dhidi ya Sudan Kusini kwa mwaka mwingine. Amnesty International inaonya mzozo unaweza kuwa mbaya zaidi iwapo marufuku haitarefushwa.

Andrew Gilmour, aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa wa Masuala ya Haki za Binadamu.
Marufuku ya Silaha dhidi ya Sudan Kusini inatarajiwa kujadiliwa katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na kuamuliwa ifikapo Mei 31.Picha: Li Muzi/imago images/Xinhua

Ulimwengu unaanza tena kuelekeza macho yake kwa Sudan Kusini, taifa changa zaidi duniani.

Kumekuwa na kuibuka kwa mzozo uliodumu kwa muda mrefu katika taifa hilo la Afrika Mashariki, ambao tayari umesababisha vifo vya maelfu ya watu, kuwafurusha watu wapatao milioni 2.3 makwao, na kuwasukuma takriban watoto 60,000 kwenye hali ya utapiamlo.

Juhudi za kimataifa za kumaliza mzozo huo zimejumuisha marufuku ya silaha iliyowekwa na Umoja wa Mataifa dhidi ya wahusika katika vita hivyo, hatua ambayo inatazamiwa kuisha Mei 31, 2025.

Kwa mujibu wa Amnesty International, maisha ya raia yako hatarini ikiwa marufuku hiyo haitarefushwa.

"Tunalihimiza Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lirefushe marufuku hiyo, lihakikishe inatekelezwa, na kulinda maisha ya raia," anasema Tigere Chagutah, Mkurugenzi wa Kanda wa Amnesty International kwa Afrika Mashariki na Kusini.

"Ingawa marufuku ya silaha ya Umoja wa Mataifa haijawa suluhisho la jumla, hali ya haki za binadamu bila hatua hiyo huenda ingekuwa mbaya zaidi,” anaongeza Tigere.

Mapigano yamezuka upya nchini Sudan Kusini kati ya vikosi tiifu kwa Rais Salva Kiir, na vile vinavyomtii makamu wake Riek Machar, na kuzusha hofu ya taifa hilo kutumbukia tena katika vita vya wenyewe kwa wenyewe.Picha: AFP

Amnesty inasema tayari kuna ukiukwaji wa wazi wa marufuku hiyo kupitia "kupelekwa kwa wanajeshi na vifaa vya kijeshi vya Uganda nchini Sudan Kusini tangu Machi 11, 2025.”

Je, kura hiyo muhimu inaweza kufanya nini wakati ukiukwaji huo uko wazi?

Mnamo Mei 30, 2024, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lilirefusha kwa mwaka mmoja vikwazo dhidi ya Sudan Kusini vilivyojumuisha kufungia mali, marufuku ya kusafiri, na marufuku ya silaha.

Wakati huo, Baraza lilisema lipo tayari kupitia upya marufuku hiyo kwa kuibadilisha, kuisitisha au kuiondoa hatua kwa hatua.

Kwa mujibu wa tathmini yake, usafirishaji wa silaha ulihusishwa na ukiukwaji wa maazimio ya kumaliza mzozo na uliendelea kuchochea hali ya kutokuwa na utulivu nchini humo.

Soma pia: Amnesty: Wanajeshi wa Uganda wamekiuka marufuku ya silaha dhidi ya Sudan Kusini

Hata hivyo, kwa mujibu wa shirika la International Crisis Group, ingawa vikwazo hivyo vinaonekana kuzuia usambazaji wa silaha nzito, mipaka isiyodhibitiwa ya nchi hiyo inafanya iwe vigumu kutekeleza marufuku dhidi ya silaha ndogo na nyepesi.

Katika barua kwa Umoja wa Mataifa mapema mwaka 2025, Makamu wa Kwanza wa Rais wa Sudan Kusini, Riek Machar, aliishtumu Uganda kwa "ukiukaji mkubwa” wa marufuku ya silaha kufuatia kupelekwa kwa vikosi vya jeshi la Uganda nchini humo—madai yanayoungwa mkono na Amnesty.

Kwa mujibu wa Amnesty, Maabara yake ya Ushahidi wa Mizozo imethibitisha video mbili zinazoonesha wanajeshi na vifaa vya Jeshi la Ulinzi wa Wananchi wa Uganda (UPDF).

"Ya kwanza inaonesha makumi ya wanajeshi wa UPDF wakifika kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Juba tarehe 11 Machi. Ya pili inaonesha magari ya kijeshi ya kubeba askari na malori ya kijeshi,” taarifa ya Amnesty imeeleza.

Miaka 10 ya Uhuru wa Sudan Kusini

01:33

This browser does not support the video element.

Katikati ya hali hii yote, kuna wasiwasi unaoongezeka kuhusu ikiwa Umoja wa Mataifa utaweza kweli kuchukua hatua dhidi ya ukiukaji huo wa wazi—na ikiwa kurefusha marufuku hiyo kutakuwa na maana yoyote katika hali hiyo.

Je, ulinzi wa amani unafanya kazi Sudan Kusini?

Hivi karibuni, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lilirefusha kwa mwaka mmoja mamlaka ya Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan Kusini (UNMISS), likieleza "wasiwasi mkubwa” kuhusu kuzorota kwa hali ya usalama nchini humo.

Pamoja na juhudi hizi zinazoendelea, baadhi ya raia wameanza kuhoji matokeo ya juhudi za kulinda amani za Umoja wa Mataifa.

Soma pia: WFP: Watoto laki 6 wakosa msaada Sudan Kusini

"Umoja wa Mataifa uko hapa Juba au maeneo mengine ya Sudan Kusini. Wapo, wanazunguka mitaani, lakini hawawezi kuchukua hatua. Wanapaswa kuwa na mamlaka ya kuingilia kati endapo kuna mapigano kati ya pande mbili—wanapaswa kuyazuia,” amesema Abraham Maliet Mamer, mchumi kutoka Mamlaka ya Uwekezaji Sudan.

"Siamini kuwa mamlaka yao yako wazi. Huwezi kusema unalinda amani, amani gani unalinda? Watu wanapigana kila siku na hujachukua hatua yoyote,” ameongeza.

Kurejea kwa Riek Machar Sudan Kusini

00:52

This browser does not support the video element.

Hata hivyo, Umoja wa Mataifa unasema unafanya kila liwezekanalo kusitisha mzozo huo.

Kamanda Mkuu wa Vikosi vya UNMISS, Luteni Jenerali Mohan Subramanian, ameiambia DW, "nchi hii imepitia vita viwili vya wenyewe kwa wenyewe kabla ya kupata uhuru na viwili baada ya uhuru wake.”

"Hakuna hamu ya mateso zaidi kwa wananchi. Wamepitia mateso makubwa kutokana na vita vya wenyewe kwa wenyewe. Kwa hiyo, tunapaswa kusitisha vita hivyo kwa gharama yoyote ile,” ameongeza.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW