1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaSudan Kusini

Sudan Kusini yaahirisha uchaguzi wa Desemba kwa miaka miwili

15 Septemba 2024

Serikali ya nchini Sudan Kusini imeahirisha uchaguzi kwa muda wa miaka miwili zaidi. Uchaguzi huo ulipangwa kufanyika mwezi Desemba mwaka huu wa 2024.

Südsudan Salva Kiir und Riek Machar
Picha: Alex McBride/AFP

Serikali imesema imeahirisha uchagzuzi huo ili kutoa nafasi ya kukamilisha michakato kama vile sensa, zoezi la kuratibu katiba ya kudumu na usajili wa vyama vya siasa.

Mshauri wa Rais kuhusu Usalama wa Kitaifa, Tut Gatluak, amesema nyongeza hiyo ya muda itatoa fursa ya kukamilishwa michakato hiyo muhimu hadi itakapotangazwa rasmi tarehe mpya ya uchaguzi ambayo ni Disemba 22, mwaka 2026.

Soma Pia: Sudan Kusini: Hakuna Mafuta, hakuna chakula

Waziri wa Masuala ya Baraza la Mawaziri, Martin Elia Lomuro, amesema hatua hiyo ya kuongeza muda imechukuliwa baada ya mapendekezo yaliyotolewa na taasisi mbili za uchaguzi na usalama.

Kushoto: Rais wa Sudan Kusini Salva Kiir. Kulia: Makamu wa Rais wa Sudan KusinibRiek MacharPicha: Peter Louis Gume/AFP

Mwezi uliopita wa Agosti, Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi nchini Sudan Kusini, Prof. Abednego Akok, aliliambia Shirika la Habari la Associated Press kuwa nchi hiyo ilikuwa nyuma ya kalenda ya uchaguzi ambapo usajili wa wapigakura ulitakiwa kuanza mwezi Juni lakini ulikuwa bado haujaanza kutokana na ukosefu wa fedha.

Sudan Kusini inakabiliwa na mzozo wa kiuchumi ambao umewaathiri watumishi wa serikali kutokana na kutolipwa mishahara kwa karibu mwaka mmoja.

Hali hiyo imesababishwa na kuathirika kwa mauzo ya nje ya mafuta baada ya bomba la kusafirishia mafuta hayo kuharibika katika nchi jirani ya Sudan iliyokumbwa na vita na ambayo Sudan Kusini inaitumia kusafirisha nje mafuta yake.

Hii ni mara ya pili kwa nchi hiyo iliyopata uhuru mwaka 2011, kuahirisha uchaguzi na kuongeza muda wa mpito ulioanza mwezi Februari mwaka 2020.

Soma Pia: Mazungumzo ya amani ya Sudan Kusini yaingia mkwamo

Rais Salva Kiir na naibu Riek Machar, ambaye zamani alikuwa mpinzani wake walitia saini makubaliano ya amani mnamo mwaka 2018 na kuvimaliza vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyodumu kwa miaka mitano. Zaidi ya watu 400,000 walikufa kwenye vita hivyo.

Mazungumzo ya Amani

Mazungumzo ya amani ya mpango wa Tumaini ambayo yamekuwa yakiendelea katika nchi jirani ya Kenya, yaliyoweka msingi wa kuyajumuisha makundi ambayo hayakutia saini makubaliano hayo pia yamekwama.

Wachambuzi wanasemaje?

Andrea Mach Mabior, mchambuzi huru wa kisiasa, ametahadharisha kwamba kufanya uchaguzi wa udanganyifu ambao haukidhi viwango vya kimataifa unaweza kusababisha upotevu wa rasilimali na machafuko.

Lakini Edmund Yakani, mkurugenzi mtendaji wa Jumuiya Shirika la Maendeleo na Uwezeshaji, kwa upande wake amesema kucheleweshwa kwa uchaguzi au kuongeza muda wa kipindi cha mpito kunaweza kusababisha vurugu katika nchi ya Sudan Kusini ambayo ni dhaifu. Yakani alliiambia shirika la Habari la AP mnamo mwezi Agosti.

"Ikiwa tutashindwa kuendesha uchaguzi mwezi Desemba, 2024 basi uwezekano wa nchi kutumbukia kwenye vurugu ni mkubwa kuliko tukiamua kuendelea na zoezi la kupiga kura."

Raia wa Sudan Kusini wanaokimbia mgogoro wa SudanPicha: LUIS TATO/AFP

Soma Pia:Riek Machar apinga mazungumzo ya Nairobi

Kulingana na makadirio ya Umoja wa Mataifa katika Muhtasari wa Mahitaji ya Kibinadamu 2024, Sudan Kusini nchi ambayo imepitia majanga ya vita vya wenyewe kwa wenyewe na maafa yanayosababishwa na mabadiliko ya hali ya hewa inahitaji msaada wa kibinadamu kwa watu wapatao milioni 9 mwaka huu wa 2024. Idadi hiyo ni sawa na asilimia 73 ya watu nchini humo.

Chanzo: AP

 

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW