Sudan kuunda serikali ya pamoja
29 Aprili 2019Chini ya makubaliano yaliyofikiwa siku ya Jumamosi, viongozi 10 wa baraza la kijeshi lililochukua madaraka baada ya kuondolewa al-Bashir watalazimika kuondoka.
Waandamanaji hao wamesema wanasubiri hatua itakayofuata kuhusu wajumbe wa baraza hilo pamoja na namna serikali hiyo ya kiraia itakavyoundwa.
Kiongozi wa maandamano, Ahmed al Rabia, amesema baraza hilo la raia na jeshi litakuwa chombo cha juu zaidi kiutawala, wakati kukisubiriwa kuundwa kwa serikali ya mpito ya kiraia.
Hapo jana, msemaji wa baraza la mpito la kijeshi, Luteni Jenerali Shams al-Deen al-Kabashi, alisema kwenye mkutano uliokutanisha wawakilishi wa pande hizo mbili kwamba makubaliano hayo yalifikiwa kwa uwazi na kila mmoja kutambua wajibu wa mwezake.
"Majadiliano yamefanyika vizuri na kwa uwazi mkubwa na pande zote mbili zimekubaliana kuhusu majukumu ya pamoja, lakini pia thamani ya taifa letu ilipewa nafasi ya juu kabisa. Kwa mapenzi ya Mungu, mazungumzo yataendelea jioni hii, na tuna matumaini sana kwamba tutapata matokeo ya mwisho yatakayotangazwa kwa watu wa Sudan haraka iwezekanavyo." alisema al-Kabashi.
Makubaliano hayo yalifikiwa baada ya mazungumzo yaliyochukua masaa kadhaa, na ya kwanza kufanywa na kamati ya pamoja inayowakilisha utawala wa sasa wa kijeshi na uongozi wa waandamanaji. Serikali ya kiraia itakuwa na jukumu la kuandaa uchaguzi.
Kimataifa, serikali za Magharibi zinaonekana kuwaunga mkono waandamanaji, lakini Saudi Arabia na Umoja wa Falme za Kiarabu zinaliunga mkono baraza hilo la kijeshi, na wiki iliyopita zilitangaza msaada wa kifedha wa dola bilioni 3 kwa baraza hilo, kufuatia kuondolewa kwa al-Bashir.
Shirika la Kimataifa la Fedha, IMF, kwa upande wake limeahidi kuendelea kuipatia Sudan misaada ya kiufundi pamoja na kisera, lakini likisema halitaendelea kutoa mikopo ya kifedha kutokana na mzigo wa madeni uliolielemea taifa hilo.
Mkurugenzi wa IMF katika eneo la Mashariki na Asia ya Kati, Jihad Azour, ameliambia shirika la habari la Reuters kwamba baraza la mpito nchini humo halijazungumzia chochote kuhusu deni linalolikabili taifa hilo, ingawa shirika hilo limeendelea kuwasiliana na mamlaka za Sudan baada ya mzozo wa sasa wa kisiasa.