Sudan: Siku ya tatu ya mapigano yapelekea vifo vya watu 97
17 Aprili 2023Mashambulizi ya anga na makombora yameendelea kushuhudiwa katika maeneo mbalimbali ya mji mkuu Khartoum na mji jirani wa Omdurman. Milio ya risasi na mabomu vilisikika pia karibu makao makuu ya jeshi, huku moshi mweupe ukionekana kutoka eneo hilo.
Wakaazi wa jiji la Khartoum wamesalia majumbani mwao huku wakiripoti pia kukatika kwa umeme na matukio kadhaa ya uporaji.
Mapigano hayo ni sehemu ya mzozo wa kugombea madaraka kati ya kamanda wa jeshi Jenerali Abdel-Fattah al-Burhan, na Jenerali Mohammed Hamdan Dagalo, mkuu wa kikundi cha kijeshi cha Rapid Support Forces (RSF).
Soma pia: Umoja wa Afrika wakutana kuijadili Sudan
Majenerali hao wawili ni washirika wa zamani ambao walipanga kwa pamoja mapinduzi ya kijeshi ya Oktoba mwaka 2021 ambayo yaliharibu mchakato wa mpito na wa muda mfupi wa Sudan kuelekea kwenye demokrasia.
Wawili hao wamekaidi na kusema hawatofikia makubaliano ya kusitisha mapigano, huku kila upande ukimtaka mwengine kujisalimisha. Hata hivyo pande zote mbili zina wafadhili wa kigeni wenye nguvu, jambo linaloweza kupelekea uwezekano mkubwa wa kusababisha shinikizo la kidiplomasia.
Tangu mapigano yalipozuka siku ya Jumamosi, raia wapatao 97 wameuawa na mamia ya wengine wamejeruhiwa, hayo ni kwa mujibu wa Shirika la Madaktari la Sudan, linalounga mkono vuguvugu la kidemokrasia na kufuatilia hali ya majeruhi. Hata hivyo, hakujakuwa na taarifa rasmi kuhusu idadi ya wapiganaji waliouawa.
Soma pia: Karibu watu 56 wauawa katika machafuko nchini Sudan
Matukio ya machafuko yaliyogubika mizinga, silaha mbalimbali na ndege za kivita katika maeneo yenye watu wengi katika mji mkuu wa Sudan, ni hali ya kutisha ambayo haijawahi kushuhudiwa huko Khartoum. Sudan ina historia ndefu ya mapigano ya wenyewe kwa wenyewe, lakini mapigano mengi yamekuwa yakifanyika katika maeneo ya kikabila na yaliyo mbali na mji wa Khartoum.
Hofu ya Jumuiya ya kimataifa
Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Antony Blinken amesema:
"Kuna wasiwasi mkubwa kwa sote kuhusu mapigano na ghasia zinazoendelea nchini Sudan. Tishio ambalo linawakabili raia na ambalo linalikabili taifa la Sudan. Tishio hilo linaweza kusambaa katika eneo zima."
Mwakilishi Maalum wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan Volker Perthes ametaja kusikitishwa na hatua ya vikosi pinzani vya kijeshi kutoheshimu kikamilifu usitishaji mapigano wa muda uliokubaliwa na pande zote hapo jana ili kuwahamisha majeruhi.
Jumuiya ya kimataifa imezitaka pande zote mbili kusitisha mapigano yaliyozuka wakati waislamu nchini humo na duniani kote wakiwa katika siku za mwisho za mafungo ya mwezi mtukufu wa Ramadhani.