Sudan, Sudan Kusini zafikia makubaliano
27 Septemba 2012Mbali na Abyei, mataifa hayo yameshindwa iua kukubaliana kuhusu maeneo mengine matano muhimu yanayoyagombania. Makubaliano hayo yenye vipengele tisa yatatiwa saini baadae hii leo (27.9.2012).
Makubaliano hayo ambayo yanategemea kuukoa uchumi wa nchi hizo mbili yamefikiwa baada ya mazungumzo ya zaidi ya wiki tatu baina ya viongozi wa mataifa hayo. Nchi hizo kwa sasa zinawajibu wa kujizuia kuingia tena katika aina yoyote ya mapigano kama yale yaliyotokea mwezi Aprili ambayo ama nusura yazirudishe kwenye vita vya wenyewe kwa wenyewe.
Wakiwa wanakabiliwa na kitisho cha vikwazo vya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa pamoja na hali ya kudorora kwa uchumi, Rais wa Sudan Omar Hassan al-Bashir na Sudan Kusini Salva Kiir hatimaye walikubaliana juu ya kuwepo kwa ukanda huo maalumu usiokuwa na shughuli za kijeshi baada ya mkutano wa kilele wa siku nne uliojadili mpango huo. Majeshi ya nchi hizo yaliyoko mpakani yatatakiwa kurudi nyuma umbali wa kilometa 10 au maili 14 kutoka eneo la mpaka.
Kuanza usafirishaji wa mafuta
Mapatano hayo yataiwezesha Sudan Kusini kusafirisha mafuta kupitia Sudan kitendo ambacho kitayapatia fedha mataifa yote mawili ambalo lilisitishwa mwezi Januari mwaka huu kutokana na kutoelewana kuhusu malipo ya usafirishaji.
Licha ya kitisho cha vikwazo na shinikizo linalozikabili nchi hizo kutoka Umoja wa Afrika, majirani hao wameshindwa kufikia muafaka juu ya maeneo matano ya mpakani yenye utajiri wa mafuta likiwemo lile la Abyei.
Licha ya kuweko kwa makubaliano hayo ambayo yatatiwa saini baadae leo, bado majirani hao wenye historia ya kuwa na mazungumzo yasiyo na mafanikio wameendelea kutoaminiana.
Msemaji wa serikali ya Sudan El-Obeid Morawah akizungumzia masuala yaliosalia alisema: "Kuna matatizo ya mpaka, maeneo yenye mzozo na yale yanayogombaniwa hivyo ni idadi kubwa ya maswali na hata kama kuna makubaliano mazuri inawezekana ikawa bado si ya kutosha kwa usuluhishi na kwa utulivu".
Aliongeza kwamaba hayo yatajadiliwa katika majadiliano ya siku zijazo huku mwenzake wa Sudan kusini Atif Kiir akisema kuwa Umoja wa Afrika ndio utakaotoa suluhu ya mwisho.
Awamu nyingine ya mazungumzo
Hata hivyo nchi hizo zimekubaliana kuwa na awamu nyingine ya mazungumzo juu ya vikwazo vilivyobakia kuhusu maeneo lakini haijawekwa wazi ni lini hasa majadiliano hayo yatafanyika. Hajafahamika pia kama yatafanyika mazungumzo zaidi leo kabla ya kutiwa saini makubaliano, au la.
Makubaliano ya usalama mpakani yatakayotiwa saini leo yatachukua miezi kuanza kutekelezwa na Sudan Kusini kuanza usafirishaji wa mafuta kutokana na njia za kusarishia nishati hiyo kujazwa maji na Sudan ili kumzuia jirani yake kuitumia mara baada ya kuokea hali ya kutokuelewana juu ya malipo ya usafirishaji. Pamoja na hayo, baadhi ya maeneo yameharibika kutokana na mapigano ya mwezi Aprili.
Awali, Umoja wa Afrika uliahirisha zoezi la kutia saini makubaliano hayo yaliyofikiwa jana ili kutoa nafasi kwa mambo mengine ambayo hayajapatiwa ufumbuzi kutatuliwa lakini hilo liligonga mwamba.
Mwandishi: Stumai George/Reuters/AFP
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman