UN inataka kuwafikia watu milioni 18 wanye uhitaji Sudan
5 Oktoba 2023Naibu mwakilishi maalum wa katibu Mkuu wa Umoja wa mataifa na Mratibu Mkazi na Misaada ya Kibinadamu nchini Sudan Clementine Nkweta-Salami, amesema wanahitaji kuwafikia watu wapatao milioni 18 na wanahitaji msaada wa kimataifa katika kufikia lengo hilo.
Ameongeza kuwausalama wao katika kufanikishashughuli zao umekuwa ni wakusuasua, huku akitaja kutokana na changamoto za kiusalama wanashindwa kufanya shughuli zao kwa kiwango kinachohitajika.
Mzozo kati ya jeshi la Sudani na vikosi vya msaada wa dharura RSF ulizuka katikati ya mwezi wa Aprili, na kusababisha mzozo mkubwa wa kibinadamu na ulioitumbukiza nchi hiyo kwenye vita vya wenyewe kwa wenyewe.
Zaidi ya watu milioni 4.2 wamekimbia makaazi yao kufuatia vita hivyo na kati ya hao takriban milioni 1.2 waliingia nchi jirani na kuongeza shinikizo la rasilimali finyu za Sudan.
Soma pia:Mataifa ya magaharibi yataka timu ya UN kuchunguza Sudan
Nkweta-Salami amesema wafanyakazi 19 wa kutoa msaada wameuwawa na wenginge 29 wamejeruhiwa tangu kuzuka kwa mapigano, jambo ambalo halikubaliki na ni kinyume cha sheria.
Ameongeza kwamba ukiritimba unatajwa kutatiza shughuli za usabambwaji wa misaada ya kiutu na ombi la msaada wa dola bilioni 2.6 kwa jumuia ya kimataifa ili kusaidia watu wa Sudani lilifadhiliwa kwa theluthi moja tu.
Aidha ametaka kukomeshwa kwa pande zote za mzozo kuingilia kati shughuli za utolewaji wa misaada, ikiwa ni pamoja na kulazimishwa kufanyiwa ukaguzi kwa malori yaliobeba msaada kadhalika kulazimishwa kwa uwepo wa jeshi wakati wa mchakato wa upakiaji huko Port Sudan na Jazeera.
WFP: Hatua za haraka zichukuliwe kumaliza njaa Sudan, Sudan Kusini
Mapema wiki hii Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani WFP nalo lilionya kwamba eneo la mpaka wa Sudan mbili likabiliwa na hali ya njaa wakati maelfu ya watu wakikimbia mapigano Sudan.
Takwimu mpya za WFP zinaonesha watu takriban 300,000ambao waliingia Sudan Kusini katika miezi mitano iliyopita, mtoto mmoja kati ya watano ana utapiamlo na asilimia 90 ya familia wanasema wanakaa siku nyingi bila kupata chakula.
Mmoja wa waathirika wa hali hiyo amesema hakuna kitu wanachoweza kufanya kwa ajili ya kujipatia chakula kutokana na changamoto walizokutana nazo baada ya kukimbia vita katika ardhi yao.
Soma pia:Watu 10 wapoteza maisha kwenye hujuma za RSF Khartoum
"Tulipokimbia khartoum tuliacha kila kitu na sasa tunateseka hapa," Alisema mama huyo huku akiwa anaendelea kupatiwa huduma ya afya kutokana na afya ya mtoto wake kutetereka.
"Afya ya mtoto wangu siwezi kufanya chochote kile kwa sababu anahitaji uangalizi wa karibu." Alisema.
Mary-Ellen McGroarty Mkurugenzi wa WFP nchini Sudan Kusini anasema Umoja wa mataifa unafanya kila linalowezekana kuokoa maisha, lakini hali bado ni mbaya.
"Tangu nimekuwa hapa nimeona hali ya watu inazidi kuzorota kwa kasi."
Alisema kundi la watu wanaovuka mpaka na kukimbia mzozo wanaendelea kuingia katika eneo hilo la mpakani na hali inaendelea kutoridhisha siku hadi siku.
"Kumwona mtoto mwenye utapiamlo mikononi mwa mama yake, bila kujua kama mtoto huyo atasalia usiku ni jambo la kustaajabisha."
Aliongeza kwamba Umoja wa Mataifa unafanya kila linalowezekana kuweza kusaidia watu hao lakini bado wanakabiliwa na changamoto chungumzima.
Umoja wa Mataifaunahofia kwamba hali inaweza kuwa mbaya zaidi ikiwa mzozo huo utaenea katika maeneo mengine kama vile jimbo la Jazeera, ambapo mapigano yanaweza kuzuia usambazaji wa chakula.