1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maandamano zaidi kufanyika wiki ijayo nchini Sudan

11 Januari 2019

Maandamano ya kuipinga serikali yaliyoanza mwezi Desemba mwaka uliopita nchini Sudan yamesababisha kuuwawa watu ishirini na mbili, idara za usalama zimesema, huku waandaaji wakiitisha maandamano upya wiki ijayo.

Sudan Rede von Präsident Omar al-Bashir
Picha: Getty Images/AFP/A. Shazly

Maandamano hayo yaliyoanza tarehe 19 Desema kufuatia uamuzi wa serikali kuongeza mara tatu bei ya mkate yameongezeka na kuwa makubwa zaidi na ambayo yanaonekana kuwa kitisho kuelekea  utawala wa miongo mitatu wa rais Bashir. Shirika la Wataalamu wa Sudan ambao ndio waandaji wa maandamano hayo, wameitisha mkutano mkubwa eneo la Khartoum Kaskazini Jumapili tarehe 13 mwezi huu, na utafuatiwa na maandamano.

Kundi hilo limeandaa maandamano leo baada ya swala ya Ijumaa kaskazini mwa mji wa Atbara. Mashirika ya kutetea haki za binadamu yamesema idadi ya waliouawa kufuatia maandamano hayo ni zaidi ya watu 22 waliothibitishwa . Jumatatu wiki hii Shirika la Human Rights Watch lilisema kwamba ni watu 40 waliouawa, wakiwemo watoto na wahudumu wa afya.

Picha: Reuters/M.N. Abdallah

Mashirika hayo pia yanasema zaidi ya watu elfu moja wamekamatwa tangu maandamano hayo yalipoanza wakiwemo viongozi wa upinzani, watetezi wa haki za binadamu, wanahabari pamoja na waandamanaji. Uingereza, Canada na Marekani zinataka chunguzi ufanywe kuhusu mauaji hayo. Mapema wiki hii katika taarifa ya pamoja nchi hizo zilionya kwamba vitendo vya Sudan huenda vikawa na athari katika uhusiano na serikali zao.

Mtafiti wa Shirika la Kimataifa la Kutetea Haki ya Kibinadamu la Amnesty International ambaye yuko jijini Nairobi Ahmed Elzobier, amesema licha ya kutowa onyo nchi hizo zinapaswa  kuchukua hatua zaidi kuidhibiti hali nchini Sudan. Ahmed amesema kwamba, ''Nadhani wanapaswa kuchukua hatua zaidi. Mojawapo ya masuala yaliyopo sasa, Umoja wa Ulaya una uhusiano wa ajabu na Sudan kuhusu suala la uhamiaji, kwa hivyo kitu wanachoweza kukifanya hasa umoja huo ni kusitisha ufadhili wa kifedha. Kwa kuwa Sudan imetajwa katika orodha ya mataifa yanayofadhili ugaidi, Marekani pia inaweza kuishinikiza Sudan kufanya mageuzi ya uongozi kwa kutumia kigezo hicho.''

Picha: Reuters/M.N. Abdallah

Wakosoaji wa Bashir wanasema usimamizi mbaya wa serikali wa sekta kuu na utumiaji mkubwa wa fedha katika kuwakabili waasi walio wachache katika eneo la Magharibi ya mji Darfur na maeneo yaliyo karibu na Sudan Kusini ndio yamechangia matatizo ya kiuchumi kwa miaka mingi.

Mwandishi: Sophia Chinyezi/AFPE

Mhariri: Saumu Yusuf