1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Sudan: Wanajeshi na upinzani kuanza tena mazungumzo

Daniel Gakuba
12 Juni 2019

Waandamanaji nchini Sudan wamekubali kusitisha kampeni ya kutotii sheria, na kurejea kwenye mazungumzo na wanajeshi. Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limezitaka pande zinazohasimiana kushirikiana kutafuta suluhu.

Sudan Khartoum - Demonstranten fordern Machtübergabe des Militär an die Bevölkerung
Picha: Reuters/Stringer

Mwafaka wa kurejea kwenye meza ya mazungumzo umetangazwa na mpatanishi kutoka Ethiopia Mahmoud Dirir, ambaye amesema vuguvugu la waandamanaji limekubali kusitisha mgomo na kutotii sheria, nalo baraza la kijeshi linalotawala Sudan likaridhia kuwaachia huru wanasiasa wa upinzani waliokuwa wametiwa kizuizini, kama ishara ya kujengeana uaminifu.

Soma zaidi: Waziri Mkuu wa Ethiopia yuko Sudan kwa juhudi za usuluhishi

Mpatanishi huyo maalumu wa Ethiopia ameyatangaza hayo usiku wa kuamkia leo, baada ya mazungumzo na pande mbili mjini Khartoum.

''Baraza la kijeshi limekubali kujenga uaminifu baina ya wadau wote. Katika juhudi hizo, litawaachia huru wafungwa wote wa kisiasa. Kwa upande wa Azimio la Uhuru na Mabadiliko, wamedhihirisha nia njema na wamekubali kusitisha zoezi la kutotii sheria.'' Amesema Dirir.

Hakuna kuangalia nyuma

Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed (kulia) ameanzisha kazi ya upatanishi katika mzozo wa SudanPicha: Reuters/M.N. Abdallah

Mpatanishi huyo amesema makubaliano haya kamwe hayatorudi nyuma, bali pande zote zinazohusika zitasonga mbele na mazungumzo pamoja na uchunguzi, katika mazingira ya uwazi na maridhiano ambayo waziri mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed aliyahimiza alipoitembelea Sudan siku za hivi karibuni.

Bado baraza la kijeshi halijatamka lolote kuhusu makubaliano yaliyotangazwa na mpatanishi huyo, Mahmoud Dirir, lakini upinzani umetoa tangazo ukiwataka watu kurejea katika shughuli zao kama kawaida.

Soma zaidi: Viongozi wa maandamano Sudan waliokamatwa waachiwa huru

Jumapili iliyopita, vuguvugu la waandamanaji liliitisha mgomo jumla na kutoheshimu sheria za umma, baada ya ukandamizaji uliofanywa na jeshi katika kuwatawanya waandamanaji tarehe 3 mwezi huu wa Juni, ambamo kulingana na duru za madaktari, watu zaidi ya 100 waliuawa.

Wananchi waliitikia mgomo huo kwa kuzifunga biashara zote na kusalia majumbani, kitendo kilichozidisha shinikizo kwa majenerali waliojitwisha jukumu la kuiongoza Sudan baada ya kuangushwa kwa utawala wa rais Omar al-Bashir Aprili 11.

Baraza la Usalama lakemea ghasia

Shinikizo kwa wanajeshi hao pia linatoka katika jumuiya ya kimataifa. Wizara ya mambo ya nje ya Marekani imetangaza kuwa mjumbe maalumu wa nchi hiyo kuhusu Afrika Tibor Nagy ameanza safari kuelekea Sudan, na anatarajiwa kukutana na viongozi wa pande mbili katika mzozo huo atakapowasili mjini Khartoum.

Nalo Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limelaani vikali ghasia zilizotokea na kutaka vurugu dhidi ya raia zisitishwe mara moja. Katika tangazo la baraza hilo baada ya kikao chake jana mjini New York, lilizihimiza pande zote kufanya kazi pamoja kutafuta suluhisho kwa mzozo unaoendelea, likitilia mkazo haja ya kuheshimu haki za binadamu na uwajibikaji kwa mujibu wa sheria.

dpae, afpe

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW