1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
JangaAfrika

Sudan yaangamia taratibu: Kipindupindu chaua 70 siku mbili

30 Mei 2025

Mlipuko mkubwa wa kipindupindu umeua watu 70 ndani ya siku mbili mjini Khartoum, Sudan – huku miundombinu ya afya ikiwa kwenye hali ya kusambaratika na mashirika ya misaada yakionya juu ya janga kubwa la afya ya umma.

Mzozo wa Sudan | Mlipuko wa kipindupindu
Mlipuko wa kipindupindu umekuwa ukijirudia tangu kuanza kwa vita kati ya jeshi la serikali na kundi la wanamgambo wa RSF, zaidi ya miaka miwili iliyopita.Picha: Zhang Meng/Xinhua News Agency/picture alliance

Mlipuko mpya wa kipindupindu umetikisa mji mkuu wa Sudan, Khartoum, na kusababisha vifo vya watu 70 ndani ya kipindi cha saa 48, hali inayoashiria janga kubwa la kiafya linaloikumba nchi hiyo iliyoathirika na vita kwa zaidi ya miaka miwili.

Wizara ya afya ya jimbo la Khartoum imeripoti kuwa siku ya Jumatano pekee kulikuwa na maambukizi mapya 942 na vifo 25, baada ya siku ya Jumanne kushuhudia visa 1,177 na vifo 45. Mlipuko huu umekuja wiki chache tu baada ya mashambulizi ya anga yanayodaiwa kufanywa na kikundi cha wanamgambo cha Rapid Support Forces, RSF, kuharibu huduma za maji na umeme jijini humo.

Khartoum imekuwa kiini cha mapigano makali kati ya jeshi la taifa na RSF tangu Aprili 2023, na miundombinu ya afya katika eneo hilo imeporomoka vibaya. Takriban asilimia 90 ya hospitali katika maeneo yaliyoathirika na vita hazifanyi kazi, hali inayozidisha changamoto za kukabiliana na mlipuko wa kipindupindu.

Miili yazidi kuanguka, misaada yabaki njia panda

Wizara ya afya ya kitaifa imesema katika wiki iliyoishia Jumanne, watu 172 walifariki kwa kipindupindu nchini Sudan, ambapo asilimia 90 ya vifo hivyo vilitokea katika jimbo la Khartoum pekee. Ingawa mamlaka zinasema asilimia 89 ya wagonjwa waliowekwa kwenye vituo vya kutenga wanapona, hali ya mazingira inazidi kudorora na kusababisha kuongezeka kwa maambukizi.

Mfumo wa afya wa Sudan umeporomoka kutokana na vita vya kikatili vinavyoendelea kati ya jeshi la taifa na kundi la RSF.Picha: Central Committee of Sudanese Doctors/AP Photo//picture alliance

Msemaji wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, António Guterres, alithibitisha kuwa chanjo dhidi ya kipindupindu zimeanza kutolewa katika eneo la Jebel Awlia, linaloathiriwa zaidi. Shirika la Afya Duniani, WHO, pia limetoa tani zaidi ya 22 za vifaa vya dharura kukabiliana na mlipuko huo.

Hata hivyo, shirika la misaada wa kiutu lam Umoja wa Mataifa, OCHA. limeonya kuhusu "tofauti kubwa" katika takwimu rasmi, hali inayofanya kuwa vigumu kutathmini ukubwa halisi wa mlipuko huu. Kipindupindu kimekuwa kikijirudia Sudan, lakini tangu kuanza kwa vita, milipuko imekuwa ya mara kwa mara na ya kushtua zaidi.

Tangu Agosti 2024, mamlaka za afya zimeorodhesha zaidi ya visa 65,000 vya kipindupindu na vifo zaidi ya 1,700 katika majimbo 12 kati ya 18 ya Sudan. Jimbo la Khartoum pekee limeshuhudia visa zaidi ya 7,700 – zaidi ya 1,000 kati yao ni watoto walio chini ya umri wa miaka mitano – na vifo 185 tangu Januari.

Mashirika yaonya kuhusu hatari ya ugonjwa kusambaa

"Sudan iko kwenye ukingo wa janga kamili la kiafya,” alisema Eatizaz Yousif, mkurugenzi wa Sudan wa shirika la International Rescue Committee. "Mchanganyiko wa vita, watu kukimbia makazi, miundombinu iliyoharibiwa na uhaba wa maji safi unaendeleza kusambaa kwa kipindupindu na magonjwa mengine hatari.”

Ufafanuzi: Je ni nchi zipi zinahusishwa na vita vya Sudan?

01:48

This browser does not support the video element.

Mashirika ya misaada yanaonya kwamba bila hatua za haraka, ugonjwa huo utasambaa zaidi pindi msimu wa mvua utakapowadia mwezi ujao, hali ambayo pia itazuia upatikanaji wa misaada ya kibinadamu.

Tangu kuanza kwa vita mnamo Aprili 2023, watu zaidi ya milioni 13 wamekimbia makazi yao nchini Sudan huku makumi ya maelfu wakipoteza maisha. Takriban watu milioni tatu walikimbia kutoka jimbo la Khartoum pekee, lakini zaidi ya 34,000 tayari wamerudi katika miezi ya hivi karibuni – wengi wao wakikuta makazi yao yameharibiwa na hawana huduma za msingi.

Kwa mujibu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto, UNICEF, zaidi ya watoto milioni moja wako kwenye hatari katika maeneo yaliyoathiriwa na kipindupindu katika jimbo la Khartoum.

Sudan sasa inahitaji msaada wa haraka – sio tu kwa ajili ya misaada ya afya, bali kwa uhai wa kizazi kizima kilichotekwa na janga la vita na maradhi.