1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Sudan yaanza kufuatilia mali zilizonyakuliwa na Bashir

1 Juni 2020

Majengo ya thamani ya mabilioni yaliyokuwa yakimilikiwa na utawala wa zamani wa rais Bashir yarudishwa mikononi mwa serikali huku hatua kabambe za kuendelea kufuatilia mali nyingine nyingi ikifanyika kote Sudan

Sudan Khartum | Prozess & Urteil Omar al-Baschir, ehemaliger Präsident | Anhänger
Picha: Getty Images/AFP/A. Shazly

Mamlaka za Sudan zimeanza kuyachukua majengo ya mabilioni ya dola yaliyomilikiwa kinyume cha sheria na utawala wa aliyekuwa kiongozi wa taifa hilo Omar al-Bashir. Kamati ya kupambana na rushwa nchini humo iliyoanza kazi mwezi Desemba inaamini kupatikana kwa mali hizo ni mwanzo wa kazi kubwa inayofuata ya kuzirudisha mali nyingi zilizopo mikononi wa Bashir zilizopatikana kwa njia isiyokuwa sahihi.

Wataalamu wanasema itakuwa vigumu baadhi ya mali kupatikana. Msemaji wa kamati iliyopewa jukumu la kupambana na rushwa na kuuvunja utawala wa zamani nchini humo Salah Manaa amesema makadirio ya awali yameonesha kwamba majengo na mali nyingine zilizomilikiwa na utawala huo wa zamani, thamani yake ni kati ya dola bilioni 3.5 mpaka 4.

Manaa ameliambia shirika la habari la AFP kwamba kilichoguswa hadi sasa ni sehemu tu ya vingi inapohusika mali jumla iliyopatikana kwa njia haramu na kufichwa chini ya utawala huo wa Bashir.

Omar Al Bashir aliitawala Sudan kwa mkono wa chuma kwa miaka 30, lakini aliondolewa kwa nguvu madarakani mnamo mwezi Aprili mwaka jana 2019 na jeshi la taifa hilo baada ya kufanyika maandamano makubwa ya wananchi walioupinga utawala wake. Kamati hii mpya ya kukabiliana na rushwa na ufisadi nchini humo ilianza kazi mwezi Desemba mwaka jana na inawajibika mbele ya serikali ya kugawana madaraka kati ya raia na majenerali wa kijeshi iliyoundwa mnamo mwezi Agosti.

Jela ya Kober anakoshikiliwa Omar BashirPicha: Getty Images/AFP

Kiongozi huyo wa zamani alishtakiwa na kuhukumiwa miaka miwili jela katika kesi mojawapo ya rushwa inayohusiana na umiliki wa fedha za kigeni kinyume cha sheria.

Ikiwa ni chini ya miezi sita tangu ilipoanza kazi kamati hiyo inazifuatilia kwa ukaribu mali za rais huyo wa zamani. Duru zimeeleza kwamba kamati hiyo ilipokea lundo la nyaraka zinazojaza malori matatu ambazo zote zitahitaji kupekuliwa na kuchunguzwa kwa makini.

Kufikia sasa wachunguzi wanaohusika wameshapata hoteli kadhaa, mashamba, maduka, ardhi za kilimo na mali nyinginezo katika mji mkuu Khartoum na miji mingine zilizokuwa zinamilikiwa na jamaa na wasaidizi wa kiongozi huyo wa zamani.

Wataalamu wa kimataifa wahitajika

Msemaji wa kamati ya kukabiliana na rushwa Salah Manaa amesema watalaamu wakimataifa watapelekwa nchini Sudan kusaidia katika shughuli ya kutathmini thamani ya mali iliyopatikana kazi ambayo hasi sasa haijafanyika isipokuwa makadirio ya dhana.

Baada ya kufanyika tathmini ya kitaalamu umiliki wa mali hizo utahamishiwa kwenye wizara ya fedha ya taifa hilo Mchambuzi  na mhariri mkuu wa gazeti la Al Tayyar la Sudan amesema kiwango cha ufisadi chini ya utawala uliopita  kilikuwa kikubwa mno na kilichotanuka.

Anaamini kwamba mtandao unaomzunguka Bashir umeficha mali nyingi kwa kutumia utaalamu ambao utahitaji muda na wataalamu kuzigundua. Moja ya changamoto kubwa inayoikabili kamati hiyo ni fedha zinazoshikiliwa na wanachama wa utawala huo wa zamani katijka mabenki kadhaa. Hata hivyo inatajwa kwamba baadhi ya mali zinazoweza kupatikana haraka huenda zikaongeza mfuko wa fedha wa kuusaidia uchumi wa taifa hilo unaoyumba.

Kwa kipindi kirefu Sudan imekabiliwa na changamoto kubwa zinazouumiza uchumi kuanzia vikwazo vya miongo kadhaa vya Marekani mpaka hatua ya kujitenga kwa eneo la utajiri mkubwa wa mafuta,Sudan Kusini mwaka 2011. Ikumbukwe kwamba hata baada ya Marekani kuoindolea nchi hiyo vikwazo kuelekea mwishoni mwa utawala wa Bashir bado nchi hiyo iko kwenye orodha ya nchi zinafadhili ugaidi hali ambayo inazuia uwekezaji.

Mwandishi: Saumu Mwasimba

Mhariri: Grace Patricia Kabogo