Sudan yaikosoa Uganda kwa kumkaribisha Dagalo
23 Februari 2026
Mohamed Hamdan Daglo alikutana na Rais Yoweri Museveni Ijumaa ya wiki iliyopita katika ikulu ya Entebbe, siku moja baada ya uchunguzi uliofanywa na Umoja wa Mataifa kugundua kwamba vikosi vyake vya RSF vilifanya uhalifu wenye viashiria vya mauaji ya kimbari katika mji wa Darfur.
Wizara ya Mambo ya Nje ya Sudan jana Jumapili iliukosoa mkutano huo ikisema ukatili uliofanywa na RSF umekuwa ukirekodiwa na jumuiya ya kimataifa na kulaaniwa na mashirika ya kikanda kama Umoja wa Afrika na Jumuiya ya ushirikiano wa maendeleo ya kiserikali kanda ya Mashariki mwa Afrika - IGAD, ambayo Uganda ni mwanachama.
Daglo 'Juhudi za amani ziongozwe na Waafrika'
Daglo, akizungumza wakati wa ziara hiyo, alisema amekwenda Uganda baada ya kuombwa na jeshi la Sudan kufanya upatanishi, huku akisisitiza juhudi za upatanishi kuongozwa na Waafrika wenyewe, alipozungumza na wafuasi wake na kuongeza kuwa walitaka iwe hivyo tangu vita hivyo vilipoanza.
Huu ni mkutano wa pili kati ya Rais Yoweri Museveni na Daglo. Mara ya kwanza walikutana mwezi Disemba 2023 wakati alipofanya ziara ya kikanda, ambayo wachambuzi walisema alikuwa akitafuta kutambuliwa na viongozi wa Afrika. Na ndipo tangu wakati huo akatangaza mamlaka kinzani huko Darfur, ambayo haijatambuliwa kimataifa hadi sasa.
Ni ziara aliyoifanya wiki moja baada ya Museveni kumwalika na kuzungumza na naibu wa Burhan katika Baraza Tawala la Mpito, Malik Agar.
Tangu Aprili 2023, jeshi la Sudan linaloongozwa na Abdel Fattah al-Burhan limekuwa likipambana na wanamgambo wa RSF wanaoongozwa na msaidizi wake wa zamani Daglo anayejulikana zaidi kama Hemeti
Juhudi za kusitisha mapigano zaendelea kusuasua
Juhudi za mara kadhaa za kusitisha mapigano hazijaweza kuzaa matunda. Mazungumzo yaliyoongozwa na Marekani, Umoja wa Falme za Kiarabu, Saudi Arabia na Misri ama Quad yamekwama kwa miezi kadhaa sasa, huku Burhan akidai kwamba kundi hilo linapendelea Umoja wa Falme za Kiarabu inayotuhumiwa kwa kuwasaidia kijeshi RSF, ingawa Abu Dhabi inakana madai hayo.
Tukiachana na mkutano huo, katika mji wa Khartoum taarifa zimesema watu tisa walikufa jana Jumapili baada ya pikipiki ya miguu mitatu ama bajaji waliyokuwa wamepanda kulipukiwa na bomu la kufukiwa ardhini. Kisa hicho kilitokea kando ya barabara iliyoko katika eneo la mapigano la Kordofan, hii ikiwa ni kulingana na chanzo cha tiba kilipozungumza na shirika la habari la AFP.
Duru kutoka hospitali ya Al-Abbasiya zimethibitisha idadi hiyo, ambapo miongoni mwao ni watoto watatu na bajaji hiyo iliharibiwa vibaya, mashuhuda wamesema.
Kordofan imekuwa kitovu cha mapigano kwenye vita vya Sudan vinavyokaribia miaka mitatu.