Sudan yajiondoa kwenye mazungumzo kuhusu mzozo wa bwawa
11 Januari 2021Misri, Sudan na Ethiopia zimetangaza kwamba zimeshindwa kufikia makubaliano katika mazungumzo yaliyosimamiwa na Umoja wa Afrika kusuluhisha mvutano kuhusu bwawa kubwa la umeme wa maji katika Mto Nile nchini Ethiopia.
Sudan imesema haitoendelea katika mazungumzo yasiyokwisha pamoja na Misri na Ethiopia baada ya kuvunjika kwa mazungumzo ya hapo Jumapili. Wiki iliopita, Misri, Sudan na Ethiopia zilikubaliana kufanya mazungumzo mapya katika matumaini ya kupata ufumbuzi wa mzozo kuhusu bwawa la umeme katika Mto Nile lililojengwa Ethiopia.
Mazungumzo yasiyokwisha ?
Shirika la habari la Sudan, Suna, limeeleza kuwa mazungumzo mapya yaliyoanza wiki iliyopita hayakuwezesha kufikiwa kwa makubaliano ya pande zote husika.
Waziri wa rasilimali za maji na umwagiliaji wa Sudan, Yasser Abbas amenukuliwa na shirika la habari la Suna akisema kuwa nchi yake haitoendelea na mazungumzo yasiokwisha, huku bwawa hilo la Ethiopia likiwa ni kitisho dhidi ya bwawa la umeme la Sudan.
Mawaziri wa nchi za nje na wa umwagiliaji wa nchi hizo, walikutana kwa mara ya pili ndani ya wiki moja kwa njia ya video katika ufumbuzi wa jinsi ya kurejea kwenye mazungumzo yao. Kwa upande wake wizara mambo ya nje ya Misri imesema nchi yake na Ethiopia zilipinga pendekezo la Sudan. Nayo wizara ya mambo ya nje ya Ethiopia imesema Sudan ilikataa pendekezo la Afrika Kusini la pande zote husika kukutana tofauti na wataalamu wa Umoja wa Afrika.
Misri yahofia uhaba wa maji ya mto Nile
Aidha, Ethiopia imesema imebuni mkakati wa kubadilishana data na Sudan kufuatia wasiwasi wa nchi hiyo kuhusu bwawa lake kwenye Mto Nile. Mnamo mwezi Novemba, Sudan ilisusia mazungumzo yaliyoitishwa na Afrika Kusini ambayo ndiyo mwenyekiti wa sasa wa Umoja wa Afrika.
Uhusiano baina ya Ethiopia na Sudan ulizorota wiki za hivi karibuni. Mapigano yaliripotiwa kwenye mpaka wa nchi mbili hizo, kufuatia operesheni za kijeshi za Ethiopia kwenye jimbo la Tigray, linalopakana na Sudan.
Ujenzi wa bwawa hilo la umeme la Ethiopia umezusha pia mivutano na Misri, nchi yenye wakaazi milioni 100 na inayotegemea maji kutoka Mto Nile kwa asilimia 97. Misri inahofia kwamba huenda mradi wa bwawa hilo ukapunguza maji ya Mto Nile.
Ethiopia iliyokumbwa na mafuriko msimu uliopita wa joto, inategemea kwamba bwawa hilo litachangia katika kuelekeza maji ya Mto Nile. Ethiopia ilitishia kwamba ikiwa hakutokuweko makubaliano yoyote basi mamilioni ya raia wake watakuwa katika hatari kubwa.