Sudan yakaidi amri ya kuwakabidhi raia wake kwa ICC
4 Juni 2008Serikali ya Sudan imeondoa uwezekano wote wa kuwakabidhi raia wake wanaoshukiwa kwa vitendo vya uhalifu katika eneo la Darfur kwa mahakama ya kimataifa ya makosa ya jinai.
Msimamo huu umetolewa huku mabalozi wa baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa wakitembelea nchi hiyo.
Ni miaka mitatu sasa tangu baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kupeleka kesi ya uhalifu wa kivita wa Darfur kwa mahakama ya kimataifa ya makosa ya jinai.
Na sasa makundi yanaotetea haki za binadamu,kwa mara nyingine tena yanalihimiza baraza hilo ambalo wajumbe wake wanazuru Sudan,kuiomba nchi hiyo iwakabidhi washukiwa wa uhalifu huo.
Shirika moja linaloitwa Justice for Darfur ambalo linayaunganisha pamoja makundi 30 ya haki za binadamu,yanataka serikali ya Khartoum ishinikizwe kuwatoa washukiwa hao.
Afisa moja wa kundi mojawapo la ushirika huo la Save the Darfur Coalition,Niemat Ahmedi, amesema kuwa huu ndio wakati kuikumbusha Sudan wajibu wake kwa mahakama ya kimataifa kwa kuwakabishi washukiwa hao.
Sudan imekuwa ikipuuza hati za kuwakamata raia wake wawili,Ahmed Haroun ambae ndie katibu wa taifa wa masuala ya kimisaada pamoja na Ali Kosheib, mkuu wa kikosi cha wanamgambo wa Janjaweed.Hati hizo zilitolewa Aprili 27 mwaka wa 2007,wakishutumiwa kufanya makosa 51 ya makosa ya kivita pamoja na makosa dhidi ya binadamu,mkiwemo visa vya mauaji,utesaji,ubakaji na pia kulazimisha watu kuhama makazi yao.
Sudan inasema kuwa iliunda mahakama yake ili kushughulikia kesi za Darfur.
Balozi wa Sudan katika Umoja wa Mataifa,Abdalmahmood Mohamad,amewaambia maripota kuwa utawala wa Khartoum hautamkabidhi rais wake yeyote kwa mahakama ya The Hague.
Amesema kuwa Sudan si mwanachama wa mahakama hiyo ya ICC,na kuwa mahakama hiyo haina ushawishi wowote na kwa serikali ya Sudan.
Ameongeza kuwa mfumo wa kimahakama wa Sudan unajulikana na kutambuliwa katika ulimwengu wa kiarabu pamoja na Afrika, na mfumo huo unalishughulikia suala la Darfur. Amesema kuwa watu wengi wamehukumiwa na wengine kunyongwa na wataendelea kuhukumiwa kuambatana na sheria za Sudan.
Mwaka jana Sudan iliiambia kamati ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa kuwa ilikuwa inashughulikia kesi zinazowakabili maafisa wakijeshi pamoja na polisi kuhusu Darfur.
Hatua hii imekuja wakati mabalaozi wa baraza la Usalama la umoja wa Mataifa wakiwa wamepangiwa kwenda Darfur kujionea wemnyewe hali ya mambo.Pia mwendesha mashtaka wa mahakama ya kimataifa Luis Moreno-Ocampo anapanga kutoa maelezo zaidi ya kesi ya pili dhidi ya maafisa wa juu waliohusika na mgogoro wa Darfur uliodumu miaka mitano.
Balozi wa Sudan katika Umoja wa Mataifa amemlaumu Ocampo na kumuita kama mwanagenzi , na kusema ndie anaeharibu juhudi za amani nchininsudan. Amesema kuwa Ocampo anaajenda yake akisema kuwa Ocampo ni mwana harakati badala ya kuwa mwanasheria.
Umoja wa Mataifa unasema kuwa takriban watu 300,000 wamepoteza maisha yao na zaidi ya milioni mbili wametoroka makazi yao tangu mgogoro wa Darfur uanze Febuari mwaka wa 2003.
Lakini serikaliya Sudan inasema kuwa watu waliokufa wanafikia tu 10,000.