Sudan yakaribisha matamshi ya Pompeo
2 Agosti 2020Pompeo mara kwa mara ameashiria kwamba wizara ya mambo ya kigeni inamatumaini ya kuondoa sifa hiyo, ambayo inazuwia kwa kiasi kikubwa uwekezaji nchini Sudan, lakini mzozo umejitokeza kuhusiana na malipo ya fidia kuhusiana na shambulizi la bomu mwaka 1998 katika balozi mbili za Marekani.
Mwanadiplomasia huyo wa ngazi ya juu wa Marekani ameiambia kamati ya mahusiano ya nje ya baraza la Seneti siku ya Alhamis kuwa sheria kuhusiana na malipo hayo yanapaswa kuwasilishwa mbele ya bunge la Marekani Congress,"katika kipindi , cha hivi karibuni kabisa".
Kwa mujibu wa ripoti kwa lugha ya Kiingereza ya shirika rasmi la habari la Sudan SUNA, serikali ya mpito ya Sudan, imekaribisha jana Jumamosi taarifa ya Pompeo na "kuahidi kufanya kila linalowezekana kutimiza mahitaji ambayo yatasaidia utawala wa Marekani "kuchukua " hatua sahihi".
Jukwaa la taarifa huru katika inteneti la Sudan Tribune limeripoti kuwa serikali imesema katika taarifa kuwa iko "tayari kuendelea kufanyakazi na utawala wa marekani kuiondoa Sudan kutoka katika orodha ya mataifa yanayofadhili ugaidi na kuingia katika uhusiano wa ushirikiano ambao utazifaidia nchi zote mbili".
Kuanguka kwa dikteta Sudan
Pompeo amesema kuwa kuanguka kwa dikteta wa muda mrefu Omar al-Bashir kufuatia maandamano makubwa na serikali inayokaribia kutimiza mwaka mmoja sasa inayoongozwa na waziri mkuu raia, Abdalla Hamdok, ni " fursa ambayo haiji mara kwa mara".
"Kuna nafasi sio tu kwa demokrasia kuanza kujengwa, lakini huenda fursa za kimkoa ambazo zitamiminika kutokana na hilo pia," amesema.
"Nafikiri kuondoa sifa ya taifa linalofadhili ugaidi nchini humo iwapo tutaweza, kuhudumia wahanga wa maafa hayo itakuwa jambo zuri kwa sera za kigeni za Marekani," Pompeo alisema.
Kwa mujibu wa shirika la habari la Sudan SUNA , Hamdok alisisitiza, "nia yake ya kuendelea kuweza juhudi pamoja na marafiki wote nchini Marekani na kwingine" kufikisha mwisho suala hilo na kwa Sudan kurejea kikamilifu kuwa "sehemu ya jumuiya ya kimataifa".
Bashir alimkaribisha kiongozi wa al-Qaeda Osama bin Laden na Sudan ilishutumiwa kusaidia wanajihadi ambao waliripua balozi nchini Kenya na tanzania, wakiwauwa watu 224 na wengine 5,000 walijeruhiwa.
Serikali mpya ya Sudan imekubali kutoa malipo ya fidia lakini mzozo umezuka kuhusiana na malipo makubwa kwa Wamarekani kuliko Waafrika, ambao idadi ya wahanga ilikuwa kubwa zaidi.