1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Sudan yakumbwa na mripuko wa ugonjwa wa kipindupindu

19 Agosti 2024

Sudan imekumbwa na mripuko wa ugonjwa wa kipindupindu ambao umesababisha vifo vya takriban watu 24 na mamia wengine kuugua katika wiki za hivi karibuni.

Mwanamume anasafisha chumba kilichotengewa wagonjwa wanaotibiwa ugonjwa wa kipindupindu katika hospitali ya Wad Al- Hilu jimboni Kassala mashariki mwa Sudan mnamo Agosti 17, 2024
Mwanamume anasafisha chumba kilichotengewa wagonjwa wanaotibiwa ugonjwa wa kipindupindu katika jimbo la Kassala mashariki mwa SudanPicha: AFP

Katika taarifa, waziri wa afya wa Sudan Haitham Mohamed Ibrahim amesema watu wasiopungua 22 wamekufa kutokana na ugonjwa huo wa kipindupindu na kwamba visa vingine 354 vilivyothibitishwa vya ugonjwa huo, pia vimegunduliwa kote nchini humo katika wiki za hivi karibuni.

Ugonjwa wa kipindupindu watangazwa kuwa janga Sudan

Siku ya Jumamosi, Ibrahim alitangaza kuwepo kwa janga la kipindupindu baada ya wiki kadhaa za mvua kubwa nchini humo.

Katika video iliyotolewa na wizara yake, Ibrahim alisema kuwa wanatangaza janga la kipindupindu kwa sababu ya hali ya hewa na kwa sababu maji ya kunywa yamechafuliwa.

WHO yasema watu 78 wamekufa kufikia Julai 28

Ibrahim hakutoa muda ambao vifo hivyo vilitokea ama hesabu ya tangu mwanzo wa mwaka, lakini Shirika la Afya Duniani WHO limesema kwamba vifo 78 vilivyosababishwa na ugonjwa huo wa kipindupindu vilirekodiwa nchini Sudan kufikia Julai 28 mwaka huu.

WHO pia imesema zaidi ya watu wengine 2400 pia waliugua kati ya Januari 1 na Julai 28.

Kiongozi wa jeshi la Sudan Abdel Fattah al-BurhanPicha: AFP

Mlipuko huo wa kipindupindu ni janga la hivi karibuni zaidi nchini Sudan, ambayo ilitumbukia katika machafuko mwezi Aprili mwaka jana wakati mvutano uliokuwa ukiendelea kati ya jeshi la nchi hilo na kundi la wanamgambo wa RSF ulipotanuka na kusababisha vita kote nchini humo.

Mzozo nchini Sudan waharibu miundombinu ya kiraia

Mzozo huo umeugeuza mji mkuu, Khartoum na maeneo mengine ya mijini kuwa viwanja vya vita na kuharibu miundombinu ya kiraia pamoja na mfumo wa huduma ya afya ambao tayari umeharibika.

Ujumbe wa serikali ya Sudan kutumwa kwa mazungumzo ya amani

Baraza huru linalodhibitiwa na jeshi la Sudan, lilisema kuwa litatuma ujumbe wa serikali kukutana na maafisa wa Marekani mjini Cairo nchini Misri huku kukiwa na shinikizo la Marekani kwa jeshi hilo kujiunga na mazungumzo ya amani yanayoendelea nchini Uswisi yanayolenga kutafuta njia ya kumaliza vita hivyo.

Soma pia:Jeshi la Sudan 'lakubali kujiunga' na mazungumzo ya Geneva

Katika taarifa, baraza hilo limesema kuwa mkutano huo wa Cairo, utaangazia utekelezwaji wa makubaliano kati ya jeshi hilo la Sudan na kundi la RSF  ambayo yanataka RSF kuondoka kwenye makazi ya watu mjini Khartoum na kwengineko nchini humo.

Soma pia:Mazungumzo ya Amani kati ya pande mbili zinazopigana Sudan kuanza tena

Mazungumzo hayo yalianza Agosti 14 nchini Uswisi na kuhudhuriwa na wanadiplomasia kutoka Marekani, Saudi Arabia, Misri, Umoja wa Falme za Kiarabu, Umoja wa Afrika na Umoja wa Mataifa. Ujumbe wa kundi la RSF ulikuwa Geneva lakini haukujiunga na mikutano hiyo.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW