Sudan yakwama tena makubaliano ya utawala wa kiraia
6 Aprili 2023![Sudan Khartoum | Abdel Fattah al-Burhan I Kusaini makubaliano](https://static.dw.com/image/63989435_800.webp)
Makubaliano ya kurejeshwa kwa utawala wa kiraia nchini Sudan yamecheleweshwa kwa mara nyingine na mazungumzo kati ya pande mbili za jeshi zinazohasimiana, hatua iliyopelekea wanaharakati wanaotetea demokrasia nchini humo kuitisha maandamano ya nchi nzima.
Sherehe za utiaji saini makubaliano hayo zilipangwa kufanyika leo Alhamis na zimeahirishwa ili kutoa nafasi kwa wanajeshi kuendelea na mazungumzo ili kumaliza tofauti zao.
Kulingana na wataalamu, suala kuu ni kujumuishwa katika jeshi kwa kikosi chenye nguvu kinachoongozwa na naibu wa kiongozi wa kijeshi, Abdel Fattah Burhan, Mohamed Hamdan Daglo.
Mapinduzi ya kijeshi ya Oktoba mwaka 2021 yalisambaratisha mchakato wa mpito uliokuwepo baada ya mapinduzi ya mwaka 2019, yaliyoung'owa utawala wa Omar al Bashir.