1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Sudan yaongeza wanajeshi Darfur baada ya vurugu.

26 Aprili 2022

Jeshi la Sudan limeongeza askari zaidi katika jimbo la Magharibi Darfur kwa lengo la kudhibiti mapigano ya kikabila ambayo yanadaiwa kusababisha mauwaji ya watu zaidi ya 175 kwa muda wa takribani siku tano zilizopita.

Sudan | UNAMID Mission
Picha: AFP

Jumapili iliyopita kulitokea makabiliano makali kati ya jamii ya Waarabu na wasio Waarabu katika mji wa Kreinik, ulio umbali wa kilometa 80 mashariki mwa mji mkuu wa jimbo la Darfur, Genena. Kimsingi mapigano hayo yaliingia hadi katika viunga vya jiji la Genena, eneo ambalo kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa serikali ilitangaza marufuku ya kutotoka nje katika nyakati za usiku.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amelaani machafuko hayo ambayo yalisababishwa na kuuliwa kwa watu wawili wa jamii ya Kiarabu na wavamizi ambao hawakuweza kufahamika mara moja. Katibu mkuu huyo pia alitoa wito wa kuharakishwa kwa upelekaji vikosi vya kulinda usalama vya ndani kwa mujibu wa makubaliano ya amani ya 2020 kati ya serikali ya Sudan na muungano wa waasi katika eneo lililoharibiwa vibaya kwa vita la Darfur.

Tangazo rasmi la nyongeza ya wanajeshi katika eneo la vita.

Vurugu katika jimbo la Darfur SudanPicha: Scott Nelson/Getty Images

Waziri wa Ulinzi wa Sudan Meja Jenerali Yassin Ibrahim Yassin alisema wanaimarisha ulinzi katika jimbo hilo na kupeleka askari kwa ajili ya kuzitenganisha pande hasimu.

Kwa mujibu wa asasi ambayo inayoratibu masuala ya ukimbizi na wasio na makaazi katika eneo la Darfur, kwa Jumapili pekee takriban watu 168 waliuawa, na wengine 89 walijeruhiwa. Na mapigano ya Alhamisi na hadi Ijumaa yalisababisha vifo vya watu 8 na 16 waliojeruhiwa.

Watoto 17 na kwanawake 27 ni miongoni mwa waliuwawa.

Tovuti ya habari katika eneo hilo ya "Darfur24" imemnukuu mkurugenzi wa halmashauri ya Kreinik, Naser al Zein, akisema waliokufa wanajumuisha watoto 17 na wanawake 27.  Ofisi ya Umoja wa Mataifa yenye kuhusika na Uratibu wa Masuala ya Kibinadamu (OCHA) imesema majengo ya serikali, kituo cha polisi na hospitali zimeshambuliwa na kuchomwa moto katika machafuko hayo yaliyodumu kwa masaa kadhaa ya Jumapili.

Mapigano hayo yalilazimu Shirika la Chakula la Umoja wa Mataifa kusimamisha usambazaji wa huduma ya chakula ambao ulipangwa kufanyika juma hili, hatua ambayo inaweza kuwaathiri takribani watu 62,850 katika mji huo pamoja na vijiji vingine vya jirani.

Soma zaidi:Kiongozi wa wapiganaji ashitakiwa ICC kwa uhalifu Darfur

Shirika la Madaktari Wasio na Mipaka lilisema katika shule ya tiba ya Genena, ambayo pia ni sehemu ya kutolea matibabu, kulifanyika mashambulizi na kusababisha kifo cha mtu mmoja na wengine kadhaa kujeruhiwa. Vurugu baina ya jamii ya Waarabu na wasio Waarabu katika mji wa Kreinik ziliwahi kutokea mwezi Desemba ambapo kwa wakati huo watu 88 waliuwawa.

Chanzo: AP

Mhariri: Mohammed Khelef

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW