1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaSudan

Sudan yapinga shutuma za kushambulia ubalozi wa UAE

30 Septemba 2024

Jeshi la Sudan limekanusha madai yaliyotolewa na jeshi la Umoja wa Falme za Kiarabu yanayosema kwamba vikosi vyake vilishambulia kwa mabomu makazi ya ubalozi wake mjini Khartoum.

Mapigano ya wenyewe kwa wenyewe
Bendera ya taifa ya Sudan imeambatishwa kwenye bunduki.Picha: Umit Bektas/REUTERS

Katika taarifa Wizara ya mambo ya nje ya Umoja wa Falme za Kiarabu imesema kwamba shambulio hilo limesababisha uharibifu mkubwa katika jengo la ubalozi wake.

Aidha wizara hiyo imesisitiza kwamba itawasilisha barua kwa Umoja wa Nchi za Kiarabu, Umoja wa Afrika na Umoja wa Mataifa dhidi ya shambulio hilo, ikidai kwamba jeshi la Sudan linawakilisha ukiukaji wa wazi wa sheria.

Soma pia: Mashambulizi ya siku mbili ya RSF huko El-Fasher yaua watu 48

Taarifa hiyo pia ilitaja umuhimu wa kulinda majengo ya kidiplomasia na makazi ya wafanyakazi wa ubalozi, kwa mujibu wa mikataba na desturi zinazodhibiti mahusiano ya kidiplomasia.

Umoja wa Falme za Kiarabu umelaani vikali kitendo hicho cha uhalifu na kukataa aina zote za unyanyasaji na ugaidi unaolenga kuharibu usalama na utulivu, kinyume na sheria za kimataifa.

Shutuma za jeshi la Sudan

Kiongozi wa kijeshi wa Sudan Jenerali Abdel Fattah al-Burhan.Picha: El Tayeb Siddig/REUTERS

Muda mfupi baada ya taarifa hiyo, Jeshi la Sudan limejibu kwa kukanusha kuhusika na shambulizi hilo na kutaja tukio hilo kama matendo ya aibu na ya woga yanafanywa na kikosi RSF.

Jeshi la Sudan limekuwa likishutumu mara kwa mara Umoja wa Falme za Kiarabu kwa kutoa silaha na msaada kwa wanamgambo wa RSF katika vita vya Sudan vilivyodumu kwa miezi 17. Madai ambayo taifa hilo la ghuba linakanusha.

Vita vilizuka mwezi Aprili mwaka jana kati ya jeshi la Sudan na vikosi vya RSF kuhusu namna ya kuondoka kwa serikali ya mpito na kuandaa uchaguzi huru.

Haya yanajiri huku juhudi za kidiplomasia zinazoongozwa na Marekani zikiendelea kudorora, huku jeshi likikataa kuhudhuria mazungumzo mwezi uliopita nchini Uswizi.

Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa karibu watu milioni 25 ambao ni nusu ya idadi jumla ya wakazi wa Sudan, wanahitaji msaada, huku baa la njaa likikaribia na watu wapatao milioni 8 wamekimbia makazi yao.

Takwimu za Shirika la Afya Ulimwenguni zinaashiria kuwa takriban watu 20,000 wameuawa katika vita vya wenyewe kwa wenyewe vinavyoendelea nchini Sudan.

 

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW