Sudan yasema mjumbe wa UN hakaribishwi tena nchini humo
9 Juni 2023Hatua hii inajiri wiki mbili tu baada ya mkuu wa majeshi wa Sudan kumtuhumu Perthes kwa kuchochea vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini humo na kutaka aondolewe.
Tangu mwisho wa mwaka jana, Perthes na ujumbe wa Umoja wa Mataifa anaouongoza katika taifa linalozongwa na machafuko la Sudan UNITAMS, wamekuwa wakilengwa na maandamano yanayoungwa mkono na jeshi na vilevile watu wenye misimamo mikali ya dini ya Kiislamu wanaolaani uingiliaji kati wa mataifa ya kigeni.
Watoto 300 wahamishiwa mahala salama, Sudan
Mwezi uliopita, kiongozi wa kijeshi wa Sudan Jenerali Abdel Fattah al-Burhan aliuandikia Umoja wa Mataifa barua, akimtuhumu Perthes kwa kuzidisha mapigano kati ya jeshi lake na wanamgambo wa kikosi chenye nguvu cha Rapid Support (RSF) kinachoongozwa na aliyekuwa naibu mkuu wa majeshi wa zamani Jenerali Mohamed Hamdan Daglo.
Ukosoaji wa Perthes wawaghadhabisha majenerali
Mara kwa mara, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amekuwa akimtetea Perthes.
Lakini viongozi wa pande mbili zinazozozana Sudan, wanaghadhabishwa na ukosoaji wa Perthes kwa kukwepa juhudi za upatanishi ili kusitisha vita na kumaliza mgogoro wa kibinadamu ambao umedumu kwa miezi miwili sasa nchini humo.
Makabiliano baina ya majeshi hasimu yapamba moto Sudan
Mnamo Alhamisi wizara ya Mambo ya Nje ya Sudan ilimwarifu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres kupitia taarifa, kwamba imemtangaza Volker Perthes kuwa mtu asiyekaribishwa tena Sudan.
Taarifa hiyo ilitolewa wakati Perthes alikuwa mjini Addis Ababa Ethiopia kwenye mfululizo wa mazungumzo ya kidiplomasia. Ujumbe anaouongoza ulisema hayo kwenye ukurasa wa Twitter.
Muda wa UNITAMS warefushwa kwa miezi 6 pekee
Wiki iliyopita, hali ya hatari ya ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan iliangaziwa katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, pale baraza hilo liliporefusha muda wa ujumbe huo wa UNITAMS kwa miezi sita pekee, tofauti na awali ambapo muda wa ujumbe huo ulirefushwa kwa mwaka mmoja.
Ujumbe wa UNITAMS uliundwa Juni 2020, kuisaidia Sudan katika juhudi zake za mpito, baada ya utawala wa aliyekuwa rais wa muda mrefu na wa kiimla Omar al-Bashir kupinduliwa mwaka mmoja uliotangulia.
Mchakato wa mpito wa kisiasa nchini Sudan ili kurejesha utawala wa kiraia ulivurugwa mwaka 2021, wakati Burhan na Daglo walikamata madaraka pamoja kabla ya kutengana.
Tangu Aprili, mapigano kati ya jeshi na wanamgambo wa RSF, yameutikisa mji mkuu Khartoum na jimbo la magharibi Darfur, licha ya makubaliano kadhaa ya kusitisha vita.
Inakadiriwa kuwa zaidi ya watu 1,800 wameuawa. Aidha Umoja wa Mataifa umeeleza kuwa watu milioni 1.2 wameyakimbia makwao huku zaidi ya watu 425,000 wakikimbilia nchi za nje.
Chanzo: AFPE