1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Sudan yasimamisha kazi za mashirika yasiokua ya kiserikali Darfur

Ramadhan Ali23 Machi 2007

Wakati huo huo Bunge la ujerumani -Bundestag laijadili hali katika jimbo hilo la magharibi mwa Sudan.

Janga la wakimbizi wa Darfur
Janga la wakimbizi wa DarfurPicha: dpa

Sudan imesimamisha kwa hivi sasa shughuli za
mashirika 52 yasio ya kiserikali nchini mwake
yanayofanya kazi mkoani Dafur.Hii imetokea wakati
mjumbe mkuu wa wa UM anaehusika na misaada ya kiutu
akianza ziara yake ya kwanza nchini humo kwa
madhumuni ya kuyapatisha mashirika hayo ya misaada
fursa bora zaidi kwa kazi zao.

Kiasi cha watu laki 2 wameuwawa katika mkoa wa Dafur
mnamo miaka 3 iliopita na zaidi ya milioni 2
wamekimbilia katika nchi jirani ya Chad .Wanamgambo wa
JANJAWEED na vikosi vya serikali wanawaandama raia
huko na ulimwengu unatumbua macho tu.
Ujerumani nayo ifanye nini ikiwa sasa mwenyekiti wa
Umoja wa Ulaya na kundi la G-8 ? Hiyo ndio mada
iliozungumzwa Alhamisi Bungeni-Bundestag huko Berlin.

Waziri mkuu wa Uingereza Tony Blair amemuandikia
Kanzela Angela Merkel wa Ujerumani kama mwenyekiti wa
sasa wa UU akimwambia wakati umewadia kumkazia kamba
rais Omar al Bashir wa Sudan. „sasa maji yamezidi
unga na hakuna cha kusubiri tena.“-msemaji wa waziri
mkuu Blair alisema.

Karibuni hivi uchunguzi wa UM umegundua kwamba mauaji
katika mkoa wa dafur sio yamekoma bali yanaendelea na
kwamba serikali mjini Khartoum imehusika moja kwa moja
katika vitendo vya kihalifu vinavyopita huko.Lakini
haikudiriki kutoka hadharani ,China na Russia zilianza
kutia munda kuzuwia ripoti hiyo kujadiliwa .

Kwa hali hii kisa cha Dafur kilipozungumzwa jana
Bungeni,Ujerumani, mbunge wa chama cha CDU Hartwig
Fischer alisema,"rai zoetu zote za kidiplomasia zimetuishia.Ikiwa
Urusi na China pamoja na nchi za kiarabu hazikun’gamua
kinachopita Dafur, basi hata Umoja wa mataifa
umeishiwa.“

Hata mbunge wa chama cha walinzi wa mazingira-chama
cha KIJANI- Bibi Kerstin Müller anaona juhudi za
kibalozi kwa sasa zimeshindwa, akaongeza kuwa, "Juhudi za kibalozi hutumika kwa bahati mbaya huku
Ulaya kuelezea kufadhahika kwake kwa kutojua la
kufanya.

Ni kweli kabisa Sudan ikiwa na kinga ya
washirika wake China na Urusi ina turufu kali
mkononi.Turufu hii lakini Sudan yaeweza tu kuicheza
kwa vile ulimwengu uliosalia haujachachama kuchukua
kitendo.Na hii yafaa kubadilika-wabunge wenzangu.“
Alidai mbunge wa chama cha Kijani Bibi Müller.
Wakati Bundestag likijadiliana, taarifa kutoka
Khartoum zinaelezea jinsi serikali ya Sudan nayo
inavyokaza kamba:

Jamal Youssef Idriss, wa Tume ya misaada ya binadamu
ya serikali .Huko Nyala, amesema mashirika yasio ya kiserikali
NGOs yamesimamishiwa shughuli zao huko Dafur baada ya
uchunguzi kugundua udanganyifu upitao huko ambao
unakiuka sheria.Akaarifu kwamba ana azma ya kukutana na mashirika yote yasio ya kiserikali yaliohusika na shughuli huko Dafur
kuzungumzia jinsi gani ya kuanzisha upya kazi zao.

John Holmes , makamo katibu mkuu wa UM anaehusika na
maswali ya misaada kwa waliofikwa na maafa amesema
amekuwa na mazungumzo ya maana sana na yenye faida
juu ya Dafur na waziri wa sudan anaehusika na maswali
ya misaada kwa waliopatwa na maafa Kosti Manibe
lakini alisisitiza hata hivyo, ni suluhisho la kisiasa
pekee ndilo litakaloleta ufumbuzi wa mgogoro wa Dafur.
Mkoa wa Dafur una opresheni kubwa kabisa hivi sasa
duniani inayojumuisha hadi watumishi 14.000-sehemu
kubwa yao ni wasudani wanaoyatumikia mashirika ya
kimataifa yasio ya kiserikali-NGOs.

Huko Juba ,rais wa kusini mwa Sudan amewataka waasi
wa mkoa wa magharibi wa Dafur kukutana katika mji
mkuu wake ili kufikia maridhiano kabla ya kuanza
mazungumzo ya amani kwa shabaha ya kukomesha uasi na
msukosuko wa maafa ya wanadamu huko.
Katika hotuba kwa mataifa fadhili huko Juba juzi,Salva
Kiir alisema pia amani nchini Sudan inabidi kujumuisha
Sudan nzima na waasi wa Dafur wanapaswa kuunda
kamati ya pamoja ili kujiandaa kwa mkutano unabidi
kufanyika mwezi ujao wa april.


Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW