1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroSudan

Sudan yautuhumu Umoja wa Falme za Kiarabu kuwasaidia RSF

29 Aprili 2024

Sudan imeomba mkutano wa dharura wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuhusu kile inachokiita "uchokozi" kutoka kwa Umoja wa Falme za Kiarabu kwa madai ya kuwasaidia wanamgambo wanaopambana na jeshi.

Wakimbizi wa Sudan
Mzozo wa Suda uliozuka mwaka mmoja uliopita umewalazimisha mamia kwa maelfu ya watu kuwa wakimbizi. Picha: Karel Prinsloo/AP/picture alliance

Kwa mujibu wa chanzo cha kidiplomasia, mwakilishi wa kudumu wa Sudan katika Umoja wa Mataifa amewasilisha ombi la kikao cha dharura cha Baraza la Usalama kujadili uchokozi wa Umoja wa Falme za Kiarabu dhidi ya watu wa Sudan, na utoaji wa silaha na vifaa kwa wanamgambo wa RSF.

Shirika rasmi la habari la nchi hiyo SUNA limethibitisha kuwa mwakilishi wa Umoja wa Mataifa wa Sudan, Al-Harith Idriss, amewasilisha ombi hilo.

Katika barua iliyoelekezwa kwa Baraza la Usalama wiki iliyopita, wizara ya mambo ya nje ya Umoja wa Falme za Kiarabu ulikataa shutuma za Sudan kwamba kusema madai hayo "yalikuwa ya uwongo na hayana msingi, wala ushahidi wowote wa kuaminika wa kuyathibitisha."

Kwa miezi kadhaa jeshi la Sudan limeshutumu Umoja wa Falme za Kiarabu kwa kuunga mkono kikosi cha wapiganaji cha RSF, madai ambayo Falme za Kiarabu inakanusha.