Sudan:Mwaka mmoja baada ya kutimuliwa Bashir
9 Aprili 2020Baada ya miezi minne ya mandamano ya kiraia kote nchini jeshi liliupindua utawala wa miaka 30 wa Bashir.
Dikteta Omar El-Bashir aliyechukuwa madaraka mwaka wa 1989 kupitia mapinduzi ya kijeshi,alihukumumiwa kwa mara ya kwanza mwezi Desemba na hivi sasa yuko gerezani mjini Khartoum.
Mmoja wa viongozi wa serikali ya mpito alielezea mwezi Februari kwamba serikali inataka kumkabidhi Bashir katika mahakama ya kimataifa ya jinai ya ICC, zaidi ya mwongo mmoja tangu waranti wa kukamatwa kwake ulipotolewa na mahakama hiyo kwa tuhuma za uhalifu dhidi ya ubindamu uliofanywa katika jimbo la Darfur, lakini utaratibu huo haujawekwa wazi.
Baada ya tofauti nyingi mwaka 2019 baina ya jeshi na viongozi wa waandamanaji, baraza la kitaifa la mpito liliundwa baina ya raia na wanajeshi ili kufuatilia serikali ya mpito kwa ajili ya uchaguzi utakaorejesha madaraka ya kiraia.
Changamoto za kipindi hicho cha mpito cha miaka mitatu ni sawa na zile zilizochangia kuanguka kwa serikali ya El-bashir, alielezea Magdi al-Gizouli,mtafiti katika taasisi ya Rift valley.
Miongoni mwa changamoto hizo ametaja, mageuzi ya kisiasa, mzozo wa kiuchumi na kuboreshwa kwa hali ya maisha ya wananchi. Mzozo sugu wa kiuchumi umedhihirika nchini Sudan, ambao umesababisha nchi hiyo kutopiga hatua kwenda mbele kufuatia miongo mitatu ya uongozi wa kimabavu.
Katika nchi hiyo ambayo kuapanda kwa bei ya mkate kulisababisha maandamano yaliyoipinduwa serikali ya Bashir, matatizo ya kiuchumi yameuweka hatarini ustawi wa kisiasa. Agosti 2019, Sudan iliunda serikali ya wasomi kufuatia makubaliano ya ugavi wa madaraka baina ya jeshi na viongozi wakuu wa upinzani.
Changa moto za serikali ya mpito
Mtaalamu wa zamani wa kiuchumi katika umoja wa mataifa, Abdallah Hamdok aliteuliwa kuwa waziri mkuu. Miongoni mwa changamoto anazokumbana nazo ni kuporomoka kwa thamani ya faranga ya Sudan kwa asilimia 70, deni kubwa la taifa hilo na mazungumzo ya amani na waasi wa Darfur, magharibi mwa nchi.
Mzozo huo uliozuka mwaka 2003 baina ya jeshi na makundi ya waasi ya kikabila ulisababisha watu laki tatu kuuliwa na wengine milioni mbili na laki tano kuyahama makaazi yao, kwa mujibu wa umoja wa mataifa.
Mwaka 2011,Sudan ambayo ilikuwa katika hali ngumu ya kiuchumi kutokana na vikwazo vya Marekani, ilijikuta pia imegawanyika kutokana na kujitenga kwa Sudan Kusini, yenye utajiri wa mafuta na iliyojitangazia uhuru wake.
Marekani iliondoa vikwazo vyake vya kiuchumi dhidi ya Sudan mwaka 2017 baada ya miaka 20, hali hiyo iliwapa matumaini viongozi wa nchi hiyo kwa ajili ya kuweko na uwekezaji kutoka nje.
Miezi ya hivi karibu serikali ya mpito ilikumbana pia na changamoto hasa za kiusalama kufuatia jaribio la mauwaji ya waziri mkuu mwezi uliopita. Huko Darfur bado makabiliano ya umwagaji damu yanaendelea baina ya makundi ya kikabila licha ya serikali kuanzisha mazungumzo na makundi ya waasi ya Kordofan kusini na Blue Nile.