Suluhu ya Cote d'Ivoire bado nusu njia
5 Januari 2011Mjumbe maalum wa Umoja wa Afrika katika mazungumzo haya ya kutatua mgogoro wa Cote d'Ivoire, Waziri Mkuu wa Kenya Raila Odinga, amewaambia waandishi wa habari mjini Nairobi kwamba, wapatanishi wanaongeza jitihada zaidi ili kuhakikisha kuwa Laurent Gbagbo anaondoka madarakani bila ya umwagikaji wa damu.
Kauli yake ya leo inakuja, baada ya sehemu ya pili ya mazungumzo kati ya wapatanishi wa ECOWAS na AU, kwa upande mmoja, na Gbagbo na Alassane Ouattara, kwa upande mwengine, yaliyofanyika wiki hii kumalizika bila ya kufikia makubaliano.
Hata hivyo, Odinga amesema kwamba, kuna dalili ya pande mbili zinazovutana, yaani Gbagbo na Ouattara, kupunguza ukali wa misimamo yao, na hivyo kutoa njia ya kuendelea zaidi kwa mazungumzo.
Odinga amewasifu Gbagbo na Ouattara kwamba ni wanasiasa wenye nguvu, lakini sasa wanaobadilisha ile misimamo yao ya awali.
"Mwanzoni Gbagbo alisisitiza iundwe kamati ya kuzihisabu upya kura, lakini tukamwambia hilo haliwezekani, kwani kura hizo ziliharibiwa na wafuasi wake. Amekubaliana nasi na yuko tayari kuendelea na majadiliano bila ya masharti yoyote. Ouattara anataka tu kizuizi alichowekewa kiondolewe na atambuliwe kama rais aliyechaguliwa na anayesubiri kuingia madarakani. Ameweka masharti hayo tu." Alisema Oginga.
Namna muendelezo wa mazungumzo unavyokwenda, baadhi ya wachambuzi wameshahitimisha kwamba itachukua muda kufikiwa kwa makubaliano rasmi ya kutatua mgogoro huu, jambo ambalo pia limethibitishwa na mwenyekiti wa sasa wa ECOWAS, Rais Goodluck Jonathan wa Nigeria, ambaye alisema hapo jana kwamba si jambo la papo kwa papo, kuweza kuutatua mgogoro wa Cote d'Ivoire.
"Ni jambo linalochukua muda pale panapokuwa na kiwango kikubwa cha kutokukubaliana katika nchi. Isitarajiwe kwamba unapokuwa na mgogoro kama huu, unarukia tu kwenye suluhisho. Inahitaji shinikizo kubwa na la muda mrefu la kimataifa kuwashawishi watu kama hawa." Alisema Rais Jonathan.
Suali linaloulizwa na wafuatiliaji wa hali ya Cote d'Ivoire hivi sasa, ni ikiwa kauli hizi za mjumbe maalum wa AU, Waziri Mkuu Odinga, na mwenyekiti wa ECOWAS, Rais Jonathan, zimeshaondosha uwezekano wa Gbagbo kuondolewa madarakani kijeshi, wazo ambalo lilionekana kupata nguvu mwanzoni mwa mgogoro huu.
Lakini, Rasi wa Kamisheni ya ECOWAS, Balozi James Victor Gbeho, anasema bado uwezekano wa kutumia nguvu za kijeshi ungalipo, kwani huo ndio msimamo halali wa ECOWAS kama ulivyotolewa mwezi Disemba.
"Lakini hata kama kuna nusu asilimia ya fursa ya kutatua mgogoro huu kwa njia za amani, basi ECOWAS na AU wataitumia."
Wakati ECOWAS na AU wakijaribu kuitumia hiyo nusu asilimia ya fursa ya kumuondoa Gbagbo kwa njia za amani, hapo jana vikosi vya Gbagbo viliyavamia makao makuu ya Democratic Party, chama cha upinzani kinachoongozwa na rais wa zamani na mgombea wa urais, Henri Konnan Beddie, na kusababisha kifo cha mtu mmoja.
Mwandishi: Mohammed Khelef/AFPE
Mhariri: Josephat Charo