Suminwa: Jeshi halikuhusika na shambulizi la Goma
13 Machi 2026
Akizungumza katika mahojiano na DW kando ya mkutano wa Umoja wa Mataifa kuhusu haki za wanawake mjini New York, Suminwa alisema serikali yake inaheshimu sheria za kimataifa za kibinadamu na haiwezi kwa makusudi kulenga wafanyakazi wa misaada.
Alisema serikali itafanya uchunguzi wa kina ili kubaini chanzo cha shambulizi hilo, ambalo waasi wa muungano wa AFC/M23 wameilaumu serikali ya Kongo. Waziri Mkuu huyo pia alitoa salamu za pole kwa familia ya mfanyakazi huyo pamoja na waathirika wengine wa tukio hilo.
"Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, kupitia serikali yake, inaeleza kwamba tunaheshimu sheria za kimataifa za kibinadamu na kwa vyovyote vile hatuwezi kujiruhusu kuwashambulia wafanyakazi wa misaada ya kibinadamu.”
AFC/M23, yadhibiti maeneo ya kimkakati
Kwa zaidi ya mwaka mmoja sasa, maeneo makubwa ya mashariki mwa Kongo yamekuwa chini ya udhibiti wa waasi wa AFC/M23, hali inayochochea mzozo wa usalama na kusababisha moja ya majanga makubwa zaidi ya kibinadamu duniani. Mamilioni ya watu wamekimbia makazi yao, huku wengine wakikosa huduma muhimu kama chakula, maji na matibabu.
Suminwa alisema kufungwa kwa viwanja vya ndege vya Goma na Bukavu kumefanya juhudi za misaada kuwa ngumu zaidi, jambo linalowaathiri hasa wanawake, watoto na wazee. Serikali ya Kongo, alisema, imekuwa ikishirikiana na mashirika ya kimataifa ili kuwezesha upatikanaji wa msaada kwa watu walio katika mazingira hatarishi.
"Tatizo kubwa tulilonalo leo ni jinsi ya kuboresha upatikanaji wa misaada ya kibinadamu kwa watu wote walio katika mazingira hatarishi.”
Mapigano yaendelea licha ya tangazo la kuyasitisha
Licha ya tangazo rasmi la kusitisha mapigano lililotolewa mwezi Februari, mapigano yanaendelea katika maeneo kadhaa. Waziri Mkuu huyo aliishutumu Rwanda na washirika wake kwa kutoheshimu makubaliano hayo, akisema serikali inalazimika kuchukua hatua za kujilinda ili kulinda mipaka na mamlaka ya nchi.
Aidha, alieleza kuwa vita vinaathiri kwa kiasi kikubwa maendeleo ya kiuchumi na kijamii ya taifa hilo. Serikali imeweka kipaumbele katika kuimarisha amani, kuunda ajira kwa vijana na kukuza uchakataji wa rasilimali ndani ya nchi ili kuimarisha uchumi wa taifa.
Suminwa amesisitiza kuwa mustakabali wa maendeleo ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo unategemea kurejeshwa kwa amani na usalama, akionya kuwa bila kusitishwa kwa vita, mateso ya raia yataendelea kuongezeka.