1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Sunak ametuliza mivutano ndani ya Conservative?

23 Oktoba 2023

Kwa kawaida, kiongozi yeyote wa kisiasa husherehekea maadhimisho ya mwaka mmoja madarakani, lakini Waziri wa Uingereza Rishi Sunak anafikia hatua hiyo wiki hii akikabiliwa na changamoto mbalimbali.

Waziri Mkuu wa Uingereza Rishi Sunak
Waziri Mkuu wa Uingereza Rishi SunakPicha: /AP/dpa/picture alliance

Sunak anafikisha mwaka mmoja mamlakani wiki hii akikabiliwa na changamoto mbalimbali huku akidhamiria pia kufanya kila aliwezalo ili asalie madarakani katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa hapo mwakani.
      
Baada ya kupoteza chaguzi mbili huku chama kikuu cha upinzani cha Labour kikiwabwaga chama cha wahafidhina, hilo lilidhihirisha ni jinsi gani Sunak, 43, ameshindwa katika kipindi cha miezi 12 ya kwanza ya uongozi wake, kufufua uwezo wa chama hicho.      
  
Tim Bale, mwandishi wa kitabu kuhusu misimamo ya mrengo wa kulia tangu Uingereza ilipojiondoa katika Umoja wa Ulaya "Brexit",  ameliambia shirika la habari la AFP kwamba: "Kadiri watu wanavyomtazama Sunak, ndivyo kwa namna fulani mapenzi yao hupungua kwake."

Aliongeza kuwa "Sunak hana kabisa haiba ya kimamlaka na hadhihirishi kama yeye ndiye kiongozi. Anaonekana kwa kiasi fulani, kutoka kwenye sera moja hadi nyingine katika jaribio la kutaka kujipendekeza kwa wapiga kura."
       
Sunak aliingia mtaa wa Downing 10 kuliko Ofisi ya Waziri Mkuu wa Uingereza mnamo Oktoba 25, 2022, baada ya kufikia tamati uongozi wa siku 49 wa Liz Truss, ambaye wakosoaji wanasema alihatarisha uchumi wa Uingereza na mustakabali wa chama chake.

Soma pia:Labour yashinda viti vya ubunge katika ngome ya Conservative Uingereza
       
Truss alimrithi Boris Johnson, ambaye alijiuzulu baada ya kukumbwa na kashfa nyingi, ikiwa ni pamoja na kutoheshimu marufuku ya kutokusanyika wakati alipoandaa sherehe katika makazi yake rasmi wakati wa janga la UVIKO-19. 

Mtaalamu wa siasa za Uingereza Richard Hayton amesema Sunak amefanikiwa kutuliza mivutano baina ya makundi kwenye chama cha Conservative na kusaidia kurejesha uaminifukwa ofisi ya waziri mkuu.

Lakini Hayton, profesa msaidizi katika Chuo Kikuu cha Leeds, ameongeza kuwa waziri huyo wa zamani wa fedha amekuwa akitatizika kuelezea maono thabiti ya uongozi wake ambayo huenda yangeweza kuwavutia wapiga kura.

Wachambuzi: Kazi zake hazijawavutia wapiga kura
 

Wakati chama cha mrengo wa kati cha Labour kikionekana kufanya vizuri katika tafiti za kura za maoni kwa zaidi ya mwaka mmoja sasa, mhadhiri wa siasa David Jeffery ameafiki kwamba kazi iliyofanywa na Sunak haikufikia malengo ya kukipiga jeki chama chake.
      
Sunak anatatizika kukamilisha vipaumbele vitano vya sera zake alivyojiwekea mnamo Januari ambavyo ni pamoja nakupunguza mfumuko wa bei, kukuza uchumi na kuzuia mashua za wahamiaji wanaovuka bahari kuingia Uingereza wakitokea nchini Ufaransa.

Viwango vya mfumuko wa bei vimefikia asilimia 6.7 huku Uingereza ikiwa na ukuaji mdogo wa kiuchumi.

Soma piaSunak kuhutubia mkutano mkuu wa Conservative:

Wahamiaji wapatao 26,000 wamewasili katika pwani ya kusini mashariki mwa Uingereza tangu kuanza kwa mwaka huu, ikiwa ni idadi ndogo kuliko mwaka jana.    
      
Baada ya kupoteza uchaguzi mdogo siku ya Alhamisi, Sunak anaonekana kukosa muelekeo kabla ya uchaguzi unaotakiwa kufanyika Januari 2025.

Waziri Mkuu wa Uingereza Rishi SunakPicha: Stefan Rousseau/Pool via REUTERS

Bale, profesa wa siasa katika Chuo Kikuu cha Queen Mary cha London amesema hii inaonyesha kana kwamba Chama cha Concervative wametumia zana zao zote kwa sasa.  

Wataalamu wengi wanasema nafasi nzuri zaidi ya Sunak kukiwezesha chama chake kupata muhula wa tano mfululizo itatokana na suala la kiuchumi ambalo litaweza kutoa ahueni kutokana na mzozo wa gharama ya maisha.

Takwimu zilizotolewa Jumatano(18.10.2023) zilionyesha kuwa kwa mara ya kwanza katika kipindi cha karibu miaka miwili, ukuaji wa mishahara nchini Uingereza ulikua juu kuliko mfumuko wa bei na hivyo kutoa mwanga wa matumaini kwa Waziri Mkuu Sunak.
      
Tumaini jingine la Sunak ni kutarajia mpasuko ndani ya chama cha Labour.

Waangalizi wanatarajia kuwa Sunak atachochea mtafaruku wa tamaduni hasa kuhusu mipango ya kupiga marufuku tiba ya uongofu kuhusu jinsia. 

Lakini Bale anashuku kuwa wapiga kura tayari wameshafanya maamuzi na kwamba Waingereza wanahitaji mabadiliko ambayo hawayaoni kwa Sunak wala chama chake cha Conservative.

Hayton ameafikiana na mtazamo huo na kusema ni vigumu kufikiria kwamba Sunak ataweza kuchukua hatua  zitakazo kizuia chama cha Labour kuwa chama kikubwa zaidi nchini Uingereza.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW