1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaUingereza

Sunak apata "pigo" katika kuwapeleka wahamiaji Rwanda

23 Januari 2024

Mpango wenye utata wa serikali ya Uingereza kuwapeleka wahamiaji nchini Rwanda umepata pigo Jumatatu, baada ya Baraza la Juu la bunge kupiga kura ili kuchelewesha kuidhinishwa kwa mkataba na serikali ya Rwanda.

England London | Rishi Sunak
Waziri Mkuu wa Uingereza Rishi SunakPicha: James Manning/AP/picture alliance

Wajumbe 214 walipiga kura kuunga mkono kucheleweshwa kuidhinishwa kwa mkataba huo dhidi ya wajumbe 171. Kwa sehemu kubwa hatua hiyo ni ya kiishara tu ingawa inaweza kuashiria upinzani zaidi unaoweza kujitokeza kwa mpango huo wa kuwapeleka wanaotafuta hifadhi katika taifa hilo la Afrika.

Ni pigo kwa Waziri Mkuu Rishi Sunak ambaye alikuwa ametoa wito kwa Baraza hilo la juu la bunge kuupitisha mpango huo akisema ndilo jambo ambalo Waingereza wanalitaka.

"Nafikiri nchi imekuwa wazi kabisa kwamba hili ni suala la kupewa kipaumbele. Tumekuwa wazi kabisa kwamba hiki ni kipaumbele. Bunge, bunge lililochaguliwa, limeunga mkono kwa wingi muswada huu," alisema Sunak.

Baraza la Juu la bunge la UingerezaPicha: Kirsty Wigglesworth/AP POOL/dpa/picture alliance

Kura ina athari ndogo kwa mchakato mzima

Wajumbe wa Baraza la Juu la Bunge la Uingereza ambao wanateuliwa badala ya kuchaguliwa, waliunga mkono hoja inayosema kwamba bunge halistahili kuidhinisha sheria hiyo hadi pale mawaziri watakapoweza kuonyesha kwamba Rwanda ni salama.

John Kerr ambaye ni mwanadiplomasia wa zamani anayeketi katika baraza hilo la juu la bunge, anasema mpango huo wa Rwanda "hauoani na majukumu yao" chini ya sheria ya kimataifa ya haki za binadamu.

Kura hiyo ina athari ndogo kwa kuwa Baraza la Juu la Bunge haliwezi kuzuia mkataba wa kimataifa na serikali inasema mkataba huo hautochelewa.

Lakini iwapo serikali itapuuza kura hiyo ya baraza la juu la bunge, hilo linaweza kutumika baadae katika kesi ya kuipinga serikali.

Rwanda imepokea mamilioni kutoka Uingereza

Sunak ameapa kusitisha uhamiaji ambao umefikia viwango vya rekodi licha ya ahadi za kufanya kuwa vigumu kuingia Uingereza hasa baada ya nchi hiyo kujiondoa kutoka kwenye Umoja wa Ulaya.

Boti ya wahamiaji katika ujia wa bahari ya UingerezaPicha: Jordan Pettitt/PA Wire/empics/picture alliance

Uingereza na Rwanda ziliingia katika makubaliano yapata miaka miwili iliyopita ambapo walikubaliana kwamba, wahamiaji wanaoingia Uingereza kupitia ujia wa bahari wa Uingereza, watapalekwa Rwanda na kusalia huko kabisa.

Uingereza imeilipa Rwanda karibu dola milioni 305 chini ya makubaliano hayo ila hakuna mtu yeyote aliyepelekwa katika nchi hiyo ya Afrika Mashariki kufikia sasa.

Mashirika ya haki za binadamu yameukosoa mpango huo kama wa kinyama na ambao hauwezi kutekelezeka. Baada ya kupingwa katika korti za Uingereza, Mahakama ya juu ya Uingereza mwezi Novemba iliamua kwamba sera hiyo ni kinyume cha sheria kwasababu Rwanda si nchi salama kwa wakimbizi.

Vyanzo: AFPE/APE

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW