Super Cup: BVB yaiangusha Bayern
4 Agosti 2019Dortmund hawajaweka siri ya kutaka kufikisha mwisho miaka saba ya ushindi wa Bayern katika Bundesliga na makamu bingwa hao wa msimu uliopita wametuma ujumbe wa mapema kwa mahasimu wao.
Mhispania Paco Alcacer alipachika bao muda mfupi tu mara timu hizo ziliporejea kutoka mapumziko kwa kiki safi kutoka nje ya sanduku la adhabu na chipukizi kutoka England Jadon Sancho alikamilisha ushindi wa Borussia Dortmund katika shambulizi la kushitukiza katika dakika ya 69.
Mabingwa wa mataji mawili katika msimu mmoja Bayern wangeweza kusawazisha muda mfupi baadaye lakini Marwin Hitz mlinda mlango wa BVB alifanikiwa kuzuwia juhudi za Kingsley Coman na Manuel Akanji aliondoa mpira uliopigwa na Thomas Mueller kabla mpira haujavuka mstari wa goli.
Kombe la shirikisho la Ujerumani duru ya kwanza ni wiki inayokuja kabla ya Bayern kufungua msimu mpya wa Bundesliga ikiwa nyumbani dhidi ya Hertha BSC Berlin hapo Agosti 16.
Sebastian Kehl , mkuu wa kitengo cha wachezaji wa Dortmund , alikiambia kituo cha utangazaji cha ZDF kwamba Super Cup ni "taji ambalo linaweza kuwapatia Dortmund msukumo, lakini timu zote mbili kwa kweli haziko katika kiwango chake cha asilimia 100. Tunafahamu kwamba bado tuna changamoto kubwa katika mashindano mbele yetu."
Dortmund ilitumia fedha nyingi hivi karibuni lakini mlinzi Nico Shulz alikuwa mchezaji pekee aliyejiunga msimu huu na makamu bingwa hao aliyeonekana katika kikosi cha kwanza.
Mlinzi Mats Hummels alikosa pambano hilo dhidi ya klabu yake ya zamani baada ya kupata maumivu mapema siku ya Jumamosi wakati Julian Brandt , Thorgan Hazard na Mateu Morey pia walikuwa nje.
Nyota wa zamani
Lakini nyota wa zamani waliokuwa mara moja walionesha uhai wakati Marco Reus alipiga kiki safi ambayo mlinda mlango Manuel Neuer wa Bayern aliuokoa kabla ya kukamilika dakika moja ya mchezo huo.
Alcacer alikuwa mara nyingi akitumika kama mchezaji wa akiba msimu uliopita lakini alitumia nafasi zake alizopata mara kadhaa na ndie alikuwa wa kwanza kufunja mlango wa Bayern.
Pasi mbovu ya Thiago iliruhusu Sancho kukatambuga upande wa wingi ya kulia na Alcacer alikutana na pasi yake na kupiga mkwaju wa chini chini uliomshinda mlinda mlango Manuel Neuer.
bayern hawakuwa na mchezaji Lucas Hernandez ambaye ni majeruhi na aliyenunuliwa kwa kitita kikubwa katika historia ya Bayern , wakati Benjamin Pavard na Fiete Arp walikuwa katika benchi. Serge Gnabry na Javi Martinez pia wamepata maumivu wakati wakiwa na kikosi chote cha zamani kilicheza msimu uliopita.
"tumeshindwa na tumesikitishwa na hilo," amesema kocha wa Bayern Nico Kovac, ambae aliongeza kwamba "hajafurahi" na uchezaji wa timu yake. "Hatukutumia nafasi tulizopata."
Kosa la Thiago halikuwa kosa pekee walilofanya wachezaji wa Bayern hata hivyo, na Dortmund walipata nafasi nzuri zaidi kabla ya kupata bao la kuongoza.
Alcacer alipiga mpira kando ya lango wakati Neuer alipokimbia kutoka golini kwake na mlinda mlango huyo wa Ujerumani pia alizuwia mpira wa Raphael Guerreiro kabla ya mapumziko.
Hitz, aliyekaa langoni badala ya Roman Burki aliyeumia , aliondoa hatari iliyoletwa na Coman wakati mchezo huo ukiwa sare ya bila kufungana na pia alizuwia juhudi za winga huyo wa Ufaransa wakati Bayern ikitafuta kusawazisha.