Suu Kyi ahukumiwa kifungo cha miaka minne jela
10 Januari 2022Duru zinazofuatilia kesi hiyo zimeeleza kuwa Suu Kyi mshindi wa Tuzo ya Amani ya Nobel amehukumiwa Jumatatu na mahakama hiyo kifungo cha miaka miwili jela kwa kosa la kuingiza kinyume cha sheria redio ndogo za mkononi za kupokea na kupeleka habari, maarufu kama walkie-talkie.
Aidha, amehukumiwa kifungo kingine cha miaka miwili kwa kosa la kukiuka sheria za idara inayosimamia majanga asilia inayohusiana na masharti ya virusi vya corona wakati akifanya kampeni. Adhabu zote hizo zitakwenda sambamba.
Hukumu ya karibuni
Hatua hiyo ni ya hivi karibuni kutokana na mfululizo wa kesi dhidi ya kiongozi huyo wa kiraia mwenye umri wa miaka 76, tangu alipoondolewa madarakani na jeshi. Mwezi Desemba, 2021, Suu Kyi alikutwa na hatia ya mashtaka mengine ya uchochezi na kukiuka taratibu za kuzuia kuenea kwa virusi vya corona na kuhukumiwa kifungo cha miaka minne jela.
Kiongozi wa kijeshi wa Myanmar, Min Aung Hlaing baadae alipunguza nusu ya adhabu hiyo na kusema kwamba anaweza kutumia kifungo chake akiwa nyumbani katika mji mkuu, Naypyidaw.
Wafuasi wa Suu Kyi wamesema kuwa mashtaka dhidi yake hayana msingi wowote na yanalenga kukomesha taaluma yake kisiasa, huku yakihalalisha hatua ya jeshi kuchukua madaraka.
Naibu Mkurugenzi wa Shirika la kimataifa la kutetea haki za binaadamu, Human Rights Watch barani Asia, Phil Robertson ameyataja mashtaka hayo kuwa ya ''uwongo na yamechochewa kisiasa''. Robertson amesema huo ni mkakati wa viongozi wa kijeshi kumuondoa katika nafasi yake moja kwa moja.
Jeshi na juhudi la kuidhibiti nchi
''Wanajaribu kuorodhesha mashtaka dhidi yake ili kuhakikisha kwamba hatoki kabisa gerezani. Nadhani wanataka kumshikilia kwa muda usiojulikana. Wanamuona kama kitisho kikubwa katika juhudi zao za kujaribu kuchukua udhibiti wa nchi na wanataka kumpa mashtaka yote wanayoweza dhidi yake,'' alifafanua Robertson.
Kesi hizo ni sehemu ya kesi nyingine kadhaa dhidi ya Suu Kyi tangu jeshi lilipochukua madaraka mwezi Februari, 2021. Iwapo atakutwa na hatia ya mashtaka yote dhidi yake anaweza kuhukumiwa kifungo cha zaidi ya miaka 100 gerezani.
Akizungumza na DW, Tin Tin Nyo, mkuu wa shirika la habari la kimataifa la Myanmar amesema mashtaka hayo yamepangwa ili kumzuia Suu Kyi kuwepo madarakani. Tin amesema jambo hilo sio la kushangaza kabisa, kwani utawala wa kijeshi unayatumia makosa hayo kama visingizio tu. Amesema Suu Kyi anawekwa mbali na wafuasi wake wa Myanmar ambao sasa wanashambuliwa na kuuawa kila siku.
Hukumu ya Suu Kyi imekosolewa kimataifa. Kamati ya Tuzo za Nobel ambayo inatoa Tuzo ya Amani ya Nobel imekosoa vikali hukumu aliyopewa Suu Kyi ikielezea wasiwasi wake kuhusu hali yake. Mwenyekiti wa kamati hiyo yenye makao yake nchini Norway, Berit Reiss-Andersen amesema hukumu hiyo imechochewa kisiasa.
Nalo shirika la kimataifa la kutetea haki za binaadamu, Amnesty International limesema katika ukurasa wake wa Twitter kwamba hukumu mpya dhidi ya Suu Kyi ni ya uonevu dhidi ya kiongozi wa kiraia. Shirika hilo limetoa wito wa kuachiwa kwa kiongozi huyo pamoja na maelfu ya watu wengine wanaoshikiliwa kinyume cha sheria tangu yalipofanyika mapinduzi ya kijeshi.
Wakati huo huo, mjumbe wa Umoja wa Mataifa anayefuatilia hali ya haki za binadamu nchini Myanmar, Thomas Andrews amesema jeshi la Myanmar linapaswa kusitisha mashambulizi kwenye mji wa Loikaw na kuondoa vizuizi kwa wale wanaojaribu kulikimbia eneo hilo. Loikaw mji mkuu wa Jimbo la Kayah linalopakana na Thailand, umekuwa ukikumbwa na mapigano makali kati ya jeshi na makundi ya waasi yanayopinga mapinduzi ya mwaka uliopita.
(AP, AFP, Reuters)