1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaAsia

Suu Kyi ahukumiwa miaka mingine 7 jela

30 Desemba 2022

Kiongozi aliyeondoshwa madarakani na jeshi nchini Myanmar, Aung San Suu Kyi, amehukumiwa kifungo chengine cha miaka saba, hukumu inayomfanya sasa kukabiliwa na zaidi ya miongo mitatu gerezani.

Thailand | Migranten aus Myanmar protestieren in Bangkok
Picha: Peerapon Boonyakiat/SOPA Images via ZUMA Press/picture alliance

Hadi hukumu hiyo ya siku ya Ijumaa (Disemba 30) inatolewa, Suu Kyi, mwenye umri wa miaka 77 na ambaye amekuwa kifungoni tangu alipopinduliwa mwaka jana, alikuwa ameshatiwa hatiani kwa kila kosa ambalo limetajwa dhidi yake na utawala wa kijeshi, yakiwemo ya ufisadi, kumiliki redio za mawasiliano, na kuvunja masharti ya kuzuia kusambaa kwa virusi vya korona.

Hukumu hiyo ya kifungo cha miaka saba ilitolewa kwa makosa matano ya ufisadi yanayohusiana na kukodi, kutengeneza na kununua helikopta kwa ajili ya waziri mmoja serikalini, ambapo alitiwa hatiani kwa "kusababisha hasara kwa serikali."

Alipopandishwa mahakamani, kiongozi huyo ambaye sasa atatumikia jumla ya miaka 33 jela kufuatia miezi 18 ya kesi dhidi yake, alionekana akiwa na afya njema, kwa mujibu wa chanzo kimoja kilichozungumza na shirika la habari la AFP.

Uamuzi wa kukata rufaa

Kwa mujibu wa chanzo hicho, ya leo ilikuwa kesi ya mwisho kwa Suu Kyi na kwamba hakuna kesi nyengine iliyosalia dhidi yake.

Waandamanaji wanaoumuunga mkono Aung San Suu Kyi nchini Thailand.Picha: Vachira Vachira/NurPhoto/picture alliance

Waandishi wa habari wamezuiwa kuhudhuria kesi hizi na mawakili wake wamekataliwa kuzungumza na vyombo vya habari.

Mwandishi wa habari wa shirika la dpa alisema barabara ya kuelekea gereza anakoshikiliwa Suu Kyi katika mji mkuu Naypyidaw ilikuwa haina vyombo vyovyote vya usafiri kabla ya kutolewa kwa hukumu hiyo.

Mmoja wa mawakili wa upande wa utetezi alisema rais wa zamani wa Myanmar, Win Myint, naye ametiwa hatiani kwa makosa hayo hayo na kuhukumiwa kifungo hicho hicho kama cha Suu Kyi, na kwamba wote wawili wangelikata rufaa. 

Kesi ya mwisho, hukumu ya mwisho

Tangu kesi dhidi yake zianze, Suu Kyi ameonekana hadharani mara moja tu kupitia picha za vyombo vya habari vya serikali akiwa mahakamani na amekuwa akitegemea mawakili wake kumfikishia ujumbe wake nje ya gereza.

Maandamano ya kumuunga mkono Aung San Suu Kyi nchini Japan.Picha: Philip Fong/AFP/Getty Images

Hukumu hii ya mwisho katika mfululizo wa kesi zake ilitolewa wakati wengi miongoni mwa waliokuwa wenzake kwenye mapambano ya demokrasia nchini Myanmar wakiwa wameamua kuachana na siasa yake ya kutumia njia za amani kwenye mapambano yao.

Badala yake, wengi wao wamemua sasa kugeukia njia ya silaha kupambana na utawala wa kijeshi wa nchi yao.

Wiki iliyopita, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa liliutolea wito utawala huo kumuachia huru Suu Kyi katika azimio lake la kwanza tangu mapinduzi ya kijeshi ya mwaka jana.

Vyanzo: AFP,dpa

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW