1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Suu Kyi aitetea Myanmar, The Hague

11 Desemba 2019

Kiongozi wa Myanmar Aung San Suu Kyi hii leo ameyakana madai ya mauaji ya kimbari dhidi ya jamii ya Waislamu walio wachache ya Rohingya yaliyofanywa na serikali ya myanmar. 

Niederlande Den Haag Aung San Suu Kyi vor dem Internationalen Gerichtshof
Picha: picture-alliance/AP Photo/P. Dejong

Aung San Suu Kyi ameyataja madai hayo kama yasiyo ya msingi na yanayopotosha. 

Aung San Suu Kyi amesema kesi hiyo haikutakiwa kusikilizwa kwenye mahakama ya juu zaidi ya kimataifa. Suu Kyi, mshindi wa tuzo ya amani ya kimataifa ya Nobeli alipozungumza mwanzoni mwa kikao cha siku tatu cha mahakama hiyo ya ICJ cha kusikiliza utetezi wa kiongozi huyo wa Myanmar, amepinga madai yaliyotolewa kwenye kesi ya msingi iliyowasilishwa na Gambia mwezi uliopita, akiituhumu Myanmar kwa kukiuka azimio la mwaka 1948 kuhusu mauaji ya kimbari. 

Suu Kyi, ambaye awali alichukuliwa na mataifa ya magharibi kama shujaa wa demokrasia, amezungumza kwa dakika 30 mbele ya jopo la majaji 17 wa mahakama hiyo mjini The Hague, akitetea hatua zilizochukuliwa na jeshi la Myanmar, ambazo kwa miaka kadhaa zilimsababishia kifungo cha nyumbani.

Majaji wa mahakama ya kimataifa ya haki, ICJPicha: Getty Images/AFP/J. Lampen

Amesema, operesheni iliyoitwa ya safishasafisha iliyoongozwa na jeshi katika jimbo lililoko magharibi mwa nchi hiyo la Rakhine iliyoanzishwa Agosti 2017, ilikuwa ni ya vikosi vya kupambana na ugaidi, dhidi ya mashambulizi ya kupangwa yaliyofanywa wanamgambo wa Rohingya kwenye vituo kadhaa vya polisi.

Kulingana na Suu Kyi, Gambia imewasilisha picha inayopotosha kuhusu uhalisia wa mambo kwenye jimbo hilo la Rakhine. "Kwa bahati mbaya sana Gambia imewasilisha mahakamani picha inayopotosha uhalisia wa hali ya mambo kwenye jimbo la Rakhine nchini Myanmar. Walakini kuna umuhimu mkubwa kwa mahakama kutathmini hali kwa kupata  ushahidi sahihi kutoka Rakhine"

Wanaharakati wa haki za binaadamu hata hivyo wanasema taarifa ya Suu Kyi inakinzana na ushahidi wa matukio yaliyotokea pamoja na madai ya mashuhuda.

Zaidi ya Warohingya 730,000 walikimbia nchi jirani Bangladesh.

Wakati kiongozi huyo wa Myanmar akikiri kwamba hatua hizo za kijeshi zilikuwa za nguvu mno na zilizosababisha mauaji ya raia, lakini amesema hazikulenga kusababisha mauaji ya halaiki, na kuongeza kuwa Myanmar ilikuwa ikichukua hatua kuwaadhibu wanajeshi waliohusika, kwa kile kilichotokea siku za nyuma.

Wakimbizi wa Rohingya waliokimbilia Bangladesh, kutoroka hatua kali za kijeshi dhidi yao.Picha: DW/A. Islam

Mwaka jana, jeshi la Myanmar lilitangaza kuwahukumu kifungo cha miaka 10 wanajeshi wake 7 kwa mauaji ya Warohingya 10 kwenye kijiji cha Inn Din, mwezi Septemba 2017, ambao hata hivyo waliachiliwa huru mapema mwaka huu, baada ya kutumikia kifungo kwa chini ya mwaka mmoja.

Wiki hii jopo hilo la majaji litasikiliza awamu ya kwanza ya shauri hilo, ambapo Gambia inaomba kuchukuliwa hatua za muda, ambayo ni sawa na zuio la mahakama dhidi ya Myanmar la kuwalinda watu wa Rohingya hadi kesi itakapomalizika kusikilizwa.

Mahakama ya ICJ haina mamlaka ya utekelezaji, lakini maamuzi yake ni ya mwisho.

Wakili wa Myanmar William Schabas ameiomba mahakama hiyo kutupilia mbali masharti hayo ya Gambia na akisema mahakama hiyo haina mamlaka hayo, lakini pia wakidai hakuna ushahidi wa kutosha kwamba kulifanyika mauaji ya kimbari. 

Takriban waandamanaji 250, raia wa Myanmar walikusanyika mbele ya mahakama ya ICJ hii leo, wakiwa na mabango yanayomuunga mkono Suu Kyi. Wanasema madai dhidi ya Myanmar ni upuuzi mtupu.

Zaidi ya Warohingya 730,000 walikimbia Myanmar hadi nchi jirani Bangladesh baada ya jeshi kuanzisha hatua kali dhidi yao. Wachunguzi wa Umoja wa Mataifa walisema watu 10,000 waliuawa.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW