Sweden yajiunga na NATO na kuwa mwanachama wa 32
8 Machi 2024Sweden imekuwa mwanachama wa 32 wa Jumuiya ya Kujihami ya NATO na kufungua ukurasa mpya baada ya karne mbili za kutoegemea upande wowote na kufikisha mwisho pia miaka miwili ya vuta ni kuvute za kidiplomasia baada ya uvamizi wa Urusi Ukraine kuleta hofu mpya. Sweden iliwasilisha nyaraka zake kwa Marekani ambayo ndiyo kiongozi wa jumuiya hiyo inayotoa ahadi ya usalama wa pamoja kwa wote. Waziri Mkuu wa Sweden Ulf Kristersson jana, alihudhuria hotuba ya hali ya taifa la Marekani ya Rais Biden kama mgeni. Katika hafla ya kukaribishwa katika jumuiya hiyo, Waziri Mkuu Kristersson ametaja kujiunga na NATO kama "hatua kubwa ila hatua ya kawaida kabisa." Ameongeza kuwa Sweden imefanya uamuzi huru na wa kidemokrasia kujiunga na jumuiya hiyo ya NATO.